Na Meleka Kulwa- Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Chalamila, amesema kuwa mmomonyoko wa maadili ni njia moja wapo ya chanzo cha rushwa.
Ameyasema hayo leo, Julai 30, 2025, katika ukumbi wa hoteli ya Mesuma jijini Dodoma, alipokuwa akifungua kikao kazi cha Kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora baina ya Taasisi simamizi za maadili na utendaji pamoja na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma, Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika kwa siku mbili, kuanzia Leo tarehe 30 hadi 31 Julai 2025.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Bw. Crispin Chalamila amesema kuwa wajibu wa kusimamia maadili ya watumishi wa umma katika utumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kudhibiti uwepo wa vitendo vya rushwa, ni suala mtambuka ambalo kisheria liko chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa mujibu wa kifungu cha 8(3)(e) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298.
Aidha, Bw. Crispin Chalamila ametoa rai kuwa tatizo la mmomonyoko wa maadili lijadiliwe kwa mapana na kuwekewa mikakati ya pamoja itakayowezesha kudhibiti uwepo wa vitendo vya rushwa katika utumishi wa umma.
Kwa upande mwingine, ameziomba taasisi zishirikiane kuwekeza katika mikakati ambayo itaakisi na kuimarisha utendaji kazi wa wataalamu wanaotoa huduma kwa wananchi, ili kwa pamoja zifikie azma ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuona kunakuwa na utumishi wa umma wenye usikivu na uwajibikaji wa hiari kwa ustawi wa wananchi wa Tanzania.
Pia amewaomba washiriki kuwasilisha majadiliano yenye ubunifu na mikakati ya kuboresha misingi ya maadili ya utendaji na maadili ya kitaaluma kama njia mojawapo ya kuimarisha utoaji wa huduma katika utumishi wa umma, na kudhibiti vitendo vya rushwa kwa lengo la kuleta ustawi kwa wananchi.
Ameziomba pia taasisi kuendeleza mawasiliano na ushirikiano baina ya taasisi simamizi za maadili pamoja na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma ili kuimarisha hali ya uadilifu katika taasisi na kuchukua hatua kwa wale wachache watakaoonekana kwenda kinyume na utaratibu uliowekwa.
Taasisi simamizi za maadili na utendaji pamoja na mamlaka simamizi za maadili ya kitaaluma, huwa zinakutana Kila mwaka kwa ajili ya Kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya maadili na utawala bora.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Felister Shuli, amesema kuwa moja ya jukumu la ofisi hiyo ni kuhakikisha maadili yanasimamiwa kwa kukuza maadili na ufuatiliaji.
Aidha, amesema kuwa kikao hicho kitasaidia taasisi simamizi na mamlaka katika taaluma kuweza kubadilishana uzoefu na taarifa katika jukumu zima la kusimamia maadili kwa watumishi wa umma.
Amesema kuwa tafiti ya mwaka 2022 inaonesha kuwa maadili kwa watumishi wa umma na wananchi umeongezeka, ambapo wananchi wanatoa taarifa za uvunjifu wa maadili kwa watumishi wa umma, na watumishi wa umma wanazingatia maadili.
“Maadili huanza na familia, yanakuja mashuleni, na makazini. Taasisi ya utumishi wa umma inasimamia mtumishi ambaye tayari ametoka kwenye familia, chuo mpaka anakuja kwenye utumishi wa umma. Swala la maadili ni endelevu, huwezi kufanya mara moja,” amesema Bi. Felister Shuli.