Na John Bukuku, Mwanza
Shirika la Under The Same Sun (UTSS) kwa kushirikiana na Village of Hope (VOH) Mwanza, limetoa taarifa kwa umma kuhusu Mnara wa Nithamini, uliopo katika Kata ya Ibisabageni, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, kuwa ni alama ya heshima, utu na upendo kwa watu wenye ualbino nchini Tanzania.
Mnara huo ulizinduliwa rasmi mwaka 2014 na Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa UTSS Canada, Bw. Peter Ash, pamoja na Vicky Ntetema, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa UTSS Tanzania, kama sehemu ya kumbukumbu kwa watu wenye ualbino waliouawa, kushambuliwa, au kuathirika kutokana na imani potofu na ushirikina.
Kwa mujibu wa UTSS, uamuzi wa kujenga mnara huo Sengerema ulitokana na historia ya eneo hilo kuwa moja ya sehemu za mwanzo nchini Tanzania kuripotiwa kwa matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino kwa lengo la kuvuna viungo vyao kwa imani za kishirikina. Mwanza, ikiwa ni sehemu ya Kanda ya Ziwa, ilikumbwa kwa kiasi kikubwa na vitendo hivyo vya kikatili, hivyo kujengwa kwa Mnara wa Nithamini ni ishara ya kupinga ukatili huo na kuhimiza elimu kuhusu ualbino na thamani ya maisha ya kila binadamu.
Mnara huo umejengwa katika mzunguko wa barabara kuu inayounganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda, hali inayoufanya kuwa sehemu ya kimkakati kufikisha ujumbe wa utu na usawa kwa watu wengi zaidi.
Katika kiini cha mnara, kuna sanamu ya chuma inayoonyesha familia yenye upendo: baba asiye na ualbino akimbeba mtoto mwenye ualbino, huku mama naye, asiye na ualbino, akimkinga mtoto huyo dhidi ya jua kwa kofia. Taswira hii inatoa ujumbe wa matumaini, usawa, na upendo kwa watu wote wenye ualbino nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.
Aidha, ardhi ambayo mnara huo umesimikwa iliwahi kutumika kwa matambiko ya kishirikina, lakini sasa imetangazwa kuwa ardhi takatifu inayomilikiwa na Yesu Kristo, kwa mujibu wa viongozi wa VOH kama shirika la Kikristo.
Takwimu za Ukatili dhidi ya Watu Wenye Ualbino Mpaka kufikia Julai 2025, Mnara wa Nithamini umeorodhesha matukio yafuatayo, Watu waliouawa ni 68, Watu walioshambuliwa ni 46 na Makaburi yaliyofukuliwa: 26
Mnara huu, ambao ni wa kwanza duniani kujengwa kwa heshima ya watu wenye ualbino, ni alama ya kitaifa na kimataifa ya kupinga ukatili, kuhimiza utu na kuelimisha jamii dhidi ya imani potofu kuhusu ualbino.
Shirika la UTSS kwa kushirikiana na VOH linaendelea kushirikiana na serikali, taasisi za kiraia, mashirika ya kidini na kimataifa, na vyombo vya habari katika kuhakikisha kuwa ujumbe wa heshima, utu na usawa unaendelea kudumu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mashirika hayo yanatoa shukrani kwa viongozi wa serikali, Sengerema Telecenter, jamii, mashirika ya dini, asasi zisizo za kiserikali, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa utamaduni na wadau wote waliowezesha juhudi za kulinda haki na maisha ya watu wenye ualbino nchini Tanzania.
“Ulinzi na haki za watu wenye ualbino ni jukumu la kila Mtanzania na kila kiongozi, kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya taifa,” imesisitizwa kwenye taarifa hiyo.