Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 umezindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 19.17 katika Wilaya ya Tabora, mkoani Tabora.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo leo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ally Usi, aliwapongeza viongozi wa Wilaya ya Tabora kwa kusimamia kwa ufanisi miradi hiyo ambayo imeidhinishwa na Mwenge wa Uhuru kuizindua rasmi.
“Uongozi wa Wilaya ya Tabora umeonyesha mfano wa kuigwa. Miradi hii imekidhi vigezo vya kitaifa na inaleta matumaini makubwa kwa wananchi,” alisema Usi.
Katika tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mheshimiwa Thomas Myinga, alimkabidhi rasmi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mheshimiwa Upendo Wella, kuendeleza mbio hizo ndani ya wilaya hiyo.
Miradi iliyozinduliwa inahusisha sekta muhimu kama elimu, afya, maji, na miundombinu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala na mikakati ya Serikali katika kuinua maisha ya wananchi wa Wilaya ya Tabora.
Wananchi walijitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo na kupongeza juhudi za Serikali, huku wakihamasishwa kushiriki katika ulinzi na uendelezaji wa miradi hiyo kwa manufaa ya jamii nzima.