Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku moja wa Tume na asasi za kiraia kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mkutano huo umefanyika leo Julai 30, 2025 Jijini Dar es Salaam. (Picha na INEC).
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku moja wa Tume na asasi za kiraia kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mkutano huo umefanyika leo Julai 30, 2025 Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg. Kailima Ramadhani. (Picha na INEC)
…………….
Na. Mwandishi Wetu
Taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu zimetakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa Tume na taasisi na asasi hizo leo Julai 30, 2025 jijini Dar es Salaam.
”Nitoe rai kwenu haswa wale mliopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hilo la kutoa elimu ya mpiga kura,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesisitiza kuwa katika kipindi cha uchaguzi Tume itafanya kazi kwa karibu na taasisi na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura.
”Niwaombe msichoke kuwasisitiza na kuwahimiza wadau na wananchi kwa ujumla kuzingatia Sheria za Uchaguzi, Kanuni na Maelekezo ya Tume. Tume nayo kwa upande wake itaendelea kuzingatia Sheria za Uchaguzi na Kanuni katika michakato yote ya uchaguzi,”amesema.
Jaji Mwambegele ameongeza kuwa wakati wa kampeni uzoefu unaonesha kuwa kunakuwa na joto la kisiasa linatokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa, hivyo ameziasa taasisi na asasi hizo kutumia nafasi yao kuwaelimisha wananchi ili uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.
”Kipindi hicho cha kampeni mnapaswa kuwahimiza wananchi kupitia majukwaa yenu kuwa makini kwa kuhakikisha kuwa hawawi chanzo cha kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu,” amesema.
Kwa mujibu wa kifungu cha 10(1)(g)(h) na (i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, Tume inao wajibu wa kutoa elimu ya mpiga kura nchini, kuratibu na kusimamia taasisi na asasi zinazotoa elimu ya mpiga kura na kualika na kusajili waangalizi wa uchaguzi.
Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu Tume imetoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa taasisi na asasi 164 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na taasisi na asasi 76 za ndani na 12 za kimataifa zimepata kibali cha uangalizi wa uchaguzi.
Baadhi ya wawakilishi wa taasisi na asasi hizo wamesema wamejipanga rasmi kutoa elimu ya mpiga kura haswa kwa vijana wanaotarajia kupiga kura kwa mara ya kwanza.
Wamesisitiza kuwa watatoa elimu kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya Tume.
Mwenyekiti wa Malezi Foundation Network, Mwalimu Neema Kabale, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa vijana walioandikishwa kuwa wapiga kura kwa mara ya kwanza wanapata uelewa wa kutosha kuhusu taratibu za kupiga kura.