Na Mwandishi Wetu, Mwanza
VIONGOZI wa klabu mbalimbali zinazoshiriki michezo ya Shirikisho la michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa Tanzania (SHIMIWI), wamepata mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu afya michezoni yaliyotolewa na Daktari bingwa kutoka taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Rocky City Mall, Jijini Mwanza.
Dkt. Eva Wakuganda, ambaye pia yupo kitengo kinachohusiana na masuala ya afya za wachezaji kwa upande wa ugonjwa wa moyo, amesema ni muhimu kupima afya kabla ya kufanya mazoezi na michezo ya aina yeyote kwa watu wazima hata kwa wanafunzi mashuleni, ili kutambua matatizo waliyonayo.
“Tunafanya hivi kwa sababu sasa kumekuwa na matatizo ya watu wazima au Watoto kuanguka wakati wakiwa kwenye michezo au mazoezi ya muda mrefu kutokana na kutokujua hitilafu ya umeme wa mioyo yao au presha za mapafu yake ni kubwa au matundu yake kupitisha hewa ni madogo na labda ni tatizo alilozaliwa nalo na kukua nalo bila kujua, na hata kunakuwa na hitilafu hata kwenye misuli na mwanamichezo anaweza kuanguka ghafla na kuzimia au kufa bila kujua ana matatizo ya moyo wakati akiwa anafanya mazoezi kwa muda mrefu, hivyo ni muhimu kupima afya zao mara kwa mara, ili kujua afya zetu mapema, ” amesema Dkt. Wakuganda.
Dkt. Wakuganda amesema matatizo ya moyo yanaongoza Duniani kwa vifo takribani milioni 20 ya watu wa rika mbalimbali, ambapo kwa takwimu za utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2021 inaonesha takribani ugonjwa huu unashika nafasi ya juu katika 10 bora za magonjwa yasiyoambukiza, lakini huweza kuepukika kwa kufanya mazoezi kiasi, kuacha kuvuta sigara, kuacha unywaji wa pombe na kula mlo kamili.
Ametoa angalizo kwa watu wazima kufanya mazoezi angalau kwa dakika 30 hadi saa moja kwa siku, kwani zaidi ya hapo unaweza kusababisha kuongezeka kwa uzito, kumea kwa sukari mwilini, mafuta kuongezeka hadi kuziba mishipa ya damu kwenye moyo, ambapo mtu akifuata masharti ya mazoezi kunasaidia kuepuka madhara hayo na magonjwa mengine, ikiwemo hatari ya kuanguka na kupoteza maisha, ambapo takwimu za Waafrika kwa mujibu wa WHO zinaonesha kati ya wanamichezo 3,000 mmojawapo anahatari ya kuanguka, tofauti na Ulaya ni kati ya 25 mmojawapo anaathari hiyo.
Amesema mbali na mafunzo haya, pia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete itatoa mafunzo zaidi kwa wanamichezo takribani 2000 watakaoshiriki kwenye michezo ya SHIMIWI inayotarajia kuanza tarehe 1-16, Septemba, 2025 kwenye viwanja mbalimbali Jijini Mwanza.
Mbali na SHIMIWI pia amesema taasisi hiyo sasa inatoa elimu ya afya kwa wanamichezo mbalimbali kwenye viwanja na maeneo yanayotumika kwa mazoezi, hususan viwanjani na gym.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Bw. Alex Temba ameishukuru taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kwa kutoa mafunzo haya kwa kuwa yatawasaidia watumishi wa umma wanapoanza mazoezi kuhakikisha wanapima afya zao, ili kuepusha madhara mbalimbali.
“Tunawakaribisha taasisi nyingine kipindi cha michezo yetu waje kutoa elimu kwa watumishi na wananchi wa Mwanza, ili ujumbe wao uweze kutufikia kwa wingi wetu, hii inasaidia serikali kwa kuwa huduma zinakuwa zimewafikia wananchi kwa haraka, hivyo rai yangu ni vyema kutambua athari za matatizo ya moyo mapema,” amesema Bw. Temba.
Naye Dkt. Richard Yomba ambaye anahusika na tiba ya michezo anayetokea Polisi amesema itambulike wazi kuwa kabla ya kufanya mazoezi au mashindano ya aina yeyote lazima mhusika akapime afya ili kutambua afya yake, kuanzia moyo na sehemu nyingine za mwili.
Dkt. Yomba ametoa ushauri kwa kuiomba taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete wawekeze elimu hii hususan kwa wanamichezo, ambao wengi wao ndio wanaoshiriki kwenye michezo mbalimbali nchini, vikiwemo vikundi vya mbio za jogging na marathoni.
“Hata mazoezi tunayofanya kwa kuangalia mikanda majumbani mwetu, au tukila chakula kwa masaa kadhaa kabla ya kwenda kwenye michezo au mazoezi au tukinywa vinywaji vya kuongeza nguvu navyo vyote vinaleta madhara kwenye moyo, hivyo tujitahidi kuhakikisha tunaepuka hayo,” amesema Dkt. Yomba.
Kwa upande wake Bi. Anna Zebedayo, mjumbe kutoka klabu ya Michezo ya mkoa wa Mwanza, amesema mafunzo hayo yawamewapa elimu itakayowasaidia wakati wanapokuwa michezoni na wachezaji wao, ambapo ameahidi kupeleka elimu hii kwa klabu yake.
“Tunaomba hawa madaktari wa taasisi ya Jakaya Kikwete waje mara kwa mara ili tuweze kupata elimu hii itayotusaidia kutambua namna mtu atakapoanguka akiwa michezoni au mazoezini anapewa huduma gani, na kujua madhara mengine mbalimbali,” amesema Bi. Anna..jpeg)
.jpeg)