Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika zenye matumizi makubwa zaidi ya pombe haramu, hali inayoleta hatari kubwa kwa afya ya umma, wataalamu wameonya.
Haya yalibainishwa leo katika mkutano uliowakutanisha wadau kutoka Serikalini na Sekta Binafsi kujadili namna ya kukabiliana na tatizo hili linalotishia maisha na kudhoofisha ukusanyaji wa mapato kutoka sekta halali ya pombe.
Mkutano huo, wenye kaulimbiu ya “Kuungana Kupambana na Pombe Haramu Nchini Tanzania,” ulisisitiza kuwa Tanzania inahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, wasimamizi wa sheria, wazalishaji, na vyombo vya sheria ili kukabili changamoto ya pombe haramu, ambayo inakadiriwa kuwa asilimia 55 ya jumla ya pombe inayozalishwa, kusambazwa na kutumiwa nchini.
“Pombe haramu bado ni suala tete nchini Tanzania. Inaleta hatari kubwa kwa afya ya umma kutokana na uzalishaji wake usiosimamiwa, ukosefu wa udhibiti wa ubora, na mara nyingi huwa na mchanganyiko hatari. Zaidi ya hayo, biashara haramu ya pombe inadhoofisha biashara halali, inanyima Serikali mapato makubwa ya kodi, na inachochea mzunguko wa uchumi usio rasmi ambao ni vigumu kuufuatilia au kuusimamia,” alibainisha Hussein Sufian, Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI).
Jukwaa hilo liliashiria uzinduzi rasmi wa utafiti wa kitaifa kuhusu pombe haramu unaolenga kubainisha ukubwa halisi na sababu za kuenea kwa pombe haramu nchini Tanzania. Aina za pombe zinazowekwa katika kundi la pombe haramu ni pamoja na bandia, pombe za kienyeji zilizotengenezwa nyumbani, pombe za magendo, pamoja na pombe zinazouzwa bila kulipa kodi za Serikali.
Utafiti huo wa pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi unatokana na mazungumzo ya awali kati ya pande hizo mbili, ambayo yalitambua umuhimu wa kuwa na ushahidi unaoungwa mkono na takwimu katika kuunda sera, kanuni na sheria za kupambana na pombe haramu nchini.
Akizungumza kwa niaba ya wazalishaji wakuu wa pombe waliohudhuria mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Obinna Anyalebechi, alisema sekta hiyo ilikuwa na shauku ya kutumia matokeo ya utafiti huo kubuni bidhaa maalum zitakazowavutia watumiaji kutoka kundi la pombe haramu kujiunga na pombe halali.
Kwa upande wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema lengo la juhudi hizi za pamoja ni kuhakikisha kuwa sera za kitaifa na hatua za udhibiti za baadaye zinatokana na ushahidi wa kuaminika unaotokana na takwimu, na kwamba watafanya kazi kwa pamoja kutafuta suluhisho endelevu na lenye manufaa kwa Watanzania na kwa sekta rasmi.
“Mkutano huu ni hatua muhimu katika kuratibu juhudi zetu za kupambana na biashara ya pombe haramu, tatizo linalohatarisha afya ya umma, kudhoofisha biashara halali, na kupunguza mapato ya Serikali,” alisema Chalamila.
Meneja wa Mradi wa Euromonitor, Benjamin Rideout, akizungumza kwenye mkutano wa wadau uliofanyika 30 Julai 2025 jijini Dar es Salaam, kujadili changamoto ya pombe haramu, inayoaminika kuchangia asilimia 55 ya matumizi ya pombe nchini. Mkutano huo uliandaliwa na CTI na kuhudhuriwa na wadau kutoka sekta binafsi na serikali. Pichani kutoka kushoto ni Prof. Lilian Kahale (UDSM), DC wa Kinondoni Mhe. Saad Mtambule, na Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Breweries, Dr. Obinna Anyalebechi.