Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imeridhishwa na hatua za ujenzi wa jengo lao jipya na namna ambavyo mkandarasi anafanya kazi kulingana na mkataba waliosaini kwani yuko mbele kwa asilimia Tatu.
Hayo yameelezwa leo Julai 31,2025 na Mwenyekiti wa Tume hiyo Profesa. John Kondolo wakati wa ziara ya ukaguzi ujenzi wa Jengo jipya la Makao yao Makuu linalojengwa katika eneo la Kilimani Jijini Dodoma ambapo linatarajiwa kuongeza fursa kwa wabunifu na kampuni atamizi, hususani kutoka Jijini Dar es Salaam, kwa kuwa na kumbi za kutosha kwa ajili ya kuendeleza ubunifu katika sayansi na teknolojia.
“Matarajio ya mkataba ni kwamba aweze kukabidhi jengo baada ya mwaka mmoja, kwa maana kwamba mwezi Machi mwaka 2026 na inatutia matumaini kwamba kwa kasi anayokwenda nayo tunaamini kwamba mwezi Machi mwakani jengo litakuwa limekamilika,”amesema.
Aidha ameongeza kuwa baada ya jengo hilo kukamilika, litakabidhiwa kwa COSTECH ambayo inasimamia masuala ya utafiti na uendeshaji wa Sayansi na Teknolojia Uvumbuzi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, jengo hilo litagharimu takribani Shilingi bilioni Nane hadi kukamilika kwake, fedha ambazo zinatolewa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza mazingira ya ubunifu na kutoa nafasi za kutosha kwa vijana na watafiti kuendeleza kazi zao.
Mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya TIL LTD, alikabidhiwa eneo la ujenzi mwezi Machi mwaka huu, na kwa mujibu wa Mhandisi Razack William kutoka kampuni hiyo, jengo hilo litakabidhiwa rasmi kwa COSTECH Machi 24, 2026, kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa miezi 12.
Kwa upande wake, Msanifu Majengo kutoka Kampuni ya Mekon Consult Ltd, Benedict Martin, ameeleza kuwa jengo hilo mbali na kuwa ofisi za makao makuu ya COSTECH, litakuwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo kumbi za wabunifu na atamizi zitakazosaidia kukuza ubunifu, hasa kwa vijana.
Ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha miundombinu ya taasisi muhimu kama COSTECH, ili kuharakisha maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia nchini.