Na WMJJWM- Dodoma
NAIBU KATIBU MKUU FELISTER ATOA WITO KWA NGOs KUTOA HUDUMA KWA JAMII. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu ametoa wito kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kutoa huduma katika jamii kama inavyotarajiwa katika utekelezaji wa majukumu yao kupitia miradi mbalimbali.
Mdemu amesema hayo Julai 31, 2025 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kilichokutanisha Mitandao ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.
Mdemu amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana nafasi kubwa ya
kufikia jamii katika maneno yao hivyo ni muhimu kuhakikisha wanaotekeleza miradi ambayo itasaidia kutoa huduma na kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
“Tuwaombe Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuendelea kutoa huduma kwa jamii kwani wao ni mkono wa pili wa Serikali katika hilo, hivyo Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa majukumu yao” amesisitiza Mdemu.
Aidha Mdemu ametoa wito kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufikisha elimu ya kirai kwa wananchi ili kuhamasisha amani na ushiriki wa raia kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili waweze kuwachagua viongozi waadilifu kwa Maendeleo ya Taifa.
“Mitandao ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yapo kila mahali na yanatekeleza dhima tofauti hivyo ni muhimu kuhamasisha amani na uzalendo kwa kila rai ana kushiriki katika uchaguzi wa viongozi kwa maendeleo yao” amesema Mdemu.
Kwa upande wake Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao amesema kikao hicho kinalenga kufanya tathmini ya utendaji wa Mashirika hayo kuelekea Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali litakalofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 13 Agosti 2025 Jijini Dodoma.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Shirika la Iringa Civil Society Organization Charles Lwabulala amepongeza Ofisi ya Msajili kwa utoaji wa huduma kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma hizo kwa njia ya mtandao jambo lililookoa gharama za ufuatiliaji na muda.