Na Philomena Mbirika, Karatu Arusha.
Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imehitimisha maadhimisho ya siku ya askari Wanyamapori duniani kwa kufanya michezo mbalimbali iliyohususu askari wa Jeshi la Uhifadhi, askari wa Jeshi la polisi wilaya ya Karatu pamoja na kufanya shughuli ya upandaji miti katika shule ya Sekondari Welwel iliyopo Karatu Mkoani Arusha.
Kamishna wa Uhifadhi NCAA ameongoza maafisa na askari katika zoezi la kupanda miti Shule ya Sekondari Welweli, kutoa elimu ya shughuli za uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa wanananchi na kuongoza watumishi hao katika michezo mbalimbali ikiwemo kukimbia kilomita tano, mchezo wa mpira wa miguu kati ya askari wa jeshi la Uhifadhi kutoka pori lla akiba Pololeti, askari walioko eneo la hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Polisi Karatu.
“NCAA ni sehemu ya Jamii, katika utekelezaji wa majukumu yetu tunashirikiana na vyombo vingine ikiwepo Polisi Wilaya za Ngorongoro na karatu pamoja na wananchi, ndio maana leo tumefanya michezo ya riadha, mazoezi yaa viungo, mchezo wa mpira wa miguu ili kuendelea kutuweka pamoja hasa katika shughuli za kuimarisha usalama na ulinzi wa rasilimali za Nchi) alifafanua Kamaishna Badru.
Badru ameeleza kuwa NCAA pia ina jukumu la kutoa elimu ya mazingira na uhifadhi shirikishi kwa jamii zinazozunguka hifadhi ya Ngorongoro, hivyo katika kuadhimisha siku ya askari wa Wanyamapori imetoaa miti bure kwa wananchi ili wakapande katika maeneo yao na kupanda miti katika shule ya Sekondari Welwel kisha kuzungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo na kuwasisitiza kutunza miti iliyopandwa pamoja na mazingira kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Katibu tawala wa Wilaya hiyo Bw. Bahati Mfungo ameipongeza NCAA kwa ushirikiano inaotoa kwa wananchi wa Wilaya ya Karatu hasa kuwapa elimu ya mazingira, upandaji miti, kupambana na mgongano kati ya Wanyamapori na wananchi pamoja na kusaidia miradi mbalimbali ya wananchi ikiwemo huduma za kijamii.
Siku ya Askari wa Wanyamapori Duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 2007 kwa lengo la kuwakumbuka askari waliopoteza maisha wakati wa kutekeleza majukumu yao, kauli mbiu ya maashimisho ya mwaka huu ni “ Rangers: Powering Transformative Conservation” ikilenga kuutambua mchango wa askari wa Wanyamapori katika kuleta mabadiliko ya kweli katika uhifadhi wa maliasili ambayo ni urithi wa Taifa.