Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Nyabundege, akimkabidhi hundi ya shilingi milioni 400,000,000 kwa ajili ya kudhamini maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nanenane) Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli,yanayotarajia kuanza Agosti Mosi katika Viwanja vya Nanenane eneo Nzuguni jijini Dodoma.
Na.Meleka Kulwa-Dodoma
KATIKA kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nanenane),ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa mikopo ya riba nafuu yenye thamani ya jumla ya Shilingi Trilioni 1.129 katika kipindi cha miaka kumi kwa lengo la kuwawezesha wakulima kiuchumi.
Akizungumza leo Julai 31,2025 jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusiana na maonyesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imejikita kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuleta mageuzi ya kilimo kwa kumkomboa mkulima wa kawaida kupitia upatikanaji wa mikopo nafuu.
“TADB inaendelea kutekeleza wajibu wake wa msingi wa kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa wakulima, kwa masharti rafiki. Lengo letu ni kuona kilimo kinakuwa cha kibiashara na chenye tija kwa maendeleo ya taifa,” amesema Bw. Nyabundege.
Bw. Nyabundege, amesema maonyesho ya mwaka huu yatakuwa ya aina yake kwa kuwa yanaashiria mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya kilimo kupitia huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa wakulima nchini.
“Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani, TADB ilikuwa na mtaji wa shilingi milioni 60, lakini mtaji huo umeongezeka kwa kiasi kubwa hadi kufikia shilingi milioni 442. Aidha, Rais Samia aliweka shilingi trilioni moja Benki Kuu ya Tanzania ili Benki Kuu izikopeshe benki za kibiashara kwa riba nafuu ya asilimia 3, na hatimaye mikopo kwa wakulima ipatikane kwa riba ya chini ya asilimia 10, ikilinganishwa na kiwango cha awali cha asilimia 20 hadi 30.”amesema
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema maonyesho ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na yanatarajiwa kutoa elimu muhimu kwa wakulima pamoja na wananchi kuhusu teknolojia, mbinu bora za kilimo na fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta ya kilimo.
“Nanenane si tu maonyesho, bali ni jukwaa la elimu, mafunzo, na uhamasishaji kwa wakulima wetu. Tunawakaribisha wadau wote kushiriki,” amesema Bw. Mweli.
Maonyesho ya Nanenane mwaka huu yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 1 Agosti, huku mgeni rasmi akiwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maonyesho hayo yatawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wakiwemo wakulima, taasisi za kifedha, watafiti, na makampuni ya pembejeo kwa lengo la kubadilishana maarifa na kuonyesha mafanikio yaliyopatikana kupitia mageuzi ya sekta ya kilimo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Julai 31,2025 jijini Dodoma kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nanenane),ambayo kitaifa yanafanyika kuanzia Agosti Mosi hadi 8 katika Viwanja vya Nanenane jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Nyabundege,akielezea mafanikio ya benki hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita ambapo benki hiyo imefadhili maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nanenane).Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Nyabundege, akimkabidhi hundi ya shilingi milioni 400,000,000 kwa ajili ya kudhamini maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nanenane) Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli,yanayotarajia kuanza Agosti Mosi katika Viwanja vya Nanenane eneo Nzuguni jijini Dodoma.