**************
Na Sixmund Begashe – Namtumbo
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuimarisha mikakati ya ulinzi wa rasilimali za Maliasili na hasa udhibiti wa Wanyamapori wakali na waharibifu katika jamii, kupitia Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS).
Hayo yamesemwa na Afisa Mhifadhi Mkuu Malikale Bi. Mwantum Haidari kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo, Wizara ya Maliasili na Utalii alipokuwa akifunga mafunzo ya kozi maalumu namba 24 ya mwaka 2025 ya VGS 110 katika Chuo cha ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii, Likuyu Sekamaganga, Mkoani Ruvuma, kwa ufadhili wa wizara ya Maliasili na Utalii.
Bi. Haidari amesema kuwa, pamoja na mikakati mingine ya ulinzi na uhifadhi wa Maliasili, Wizara inaendelea kushirikisha jamii katika kuhakikisha changamoto ya migogoro ya Wanyamapori wakali na waharibifu inadhibitiwa ili wananchi waendele kuishi kwa amani na kujiongezea kipato kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo.
Licha ya kuwapongeza wahitimu hao, pia aliwaasa kuyatumia mafunzo waliyopata kuongeza nguvu katika ulinzi wa rasilimali za maliasili na hasa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika jamii na si vinginevyo.
“Ni imani yangu kuwa mtakuwa walimu wazuri kwenye jamii zenu kwa kuwafundisha mbinu za kudhibiti wanyamapori ambazo ni rafiki katika mazingira yenu ili jamii nzima iweze kuzitumia kwa Uhifadhi endelevu”. Alisema Bi. Haidari
Aidha Bi. Haidari amekipongeza Chuo hicho kwa kazi nzuri ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za uhifadhi endelevu wa Maliasili kwa kutoa mafunzo kwa VGS ambao wana mchango mkubwa katika kuwalinda wananchi na mali zao dhidi ya Wanyamapori wakali na waharibifu.
Naye Mkuu wa Chuo cha Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii, Likuyu Sekamaganga, Bi. Jane Nyau amesema askari waliohitimu mafunzo hayo wametoka katika Halmashauri za Wilaya 23 zenye changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu ambazo ni; Bariadi, Busega, Handeni, Iringa, Itilima Karagwe, Kilosa, Kilwa, Lindi
Wilaya nzingine ni pamoja na Lindi, Liwale, Lushoto, Malinyi, Manyoni, Meatu, Morogoro, Namtumbo, Nkasi, Ruangwa, Rufiji, Sikonge, Songwe , na Tunduru.