Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Julai 31,2025.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg Kailima Ramadhani akitoa mada wakati wa Kikao cha Tume na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kuhusu uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Kikao hicho cha siku moja kilifanyika jijini Dar es Salaam leo Julai 31,2025.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)
imeyataka makundi mbalimbali ya kijamii nchini kuyatumia majukwaa yao
kuwahamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Wito huo umetolewa leo, tarehe 31 Julai
2025, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mheshimiwa Jaji wa
Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, wakati akifungua mkutano kati ya Tume na
wawakilishi wa watu wenye ulemavu.
Katika hotuba yake, Jaji Mwambegele ameeleza
kuwa Tume inatambua na kuthamini mchango wa watu wenye ulemavu katika kueneza
taarifa sahihi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi.
“Nawasihi kutumia majukwaa yenu kuhimiza
wenzenu kushiriki kwa amani na kuepuka kauli au vitendo vinavyoweza kuhatarisha
utulivu wa nchi yetu wakati wa kampeni,” amesema Mhe. Mwambegele, na kuongeza
kuwa Tume itaendelea kushirikiana nao katika hatua zote muhimu kuelekea
uchaguzi.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi
mkuu, Jaji Mwambegele amesema kuwa ratiba rasmi imeshatangazwa ambapo utoaji wa
fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi mbalimbali utafanyika kuanzia tarehe 9
Agosti hadi 27 Agosti 2025, huku kampeni zikipangwa kuanza tarehe 28 Agosti
hadi 28 Oktoba 2025 kwa upande wa Tanzania Bara.
Katika mkutano mwingine na wawakilishi
wa wanawake uliofanyika pia jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Tume,
Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk, amewahimiza
wanawake kutumia nafasi zao kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu hatua
za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, na kuhamasisha waliojiandikisha kwenye Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
Aidha, Jaji Mbarouk ametoa pongezi kwa
wanawake kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kilichoanza tarehe 20 Julai 2024
na kukamilika tarehe 4 Julai 2025.
“Natoa pongezi kwenu kwa namna
mlivyotuunga mkono wakati wote wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura. Tunawapongeza na tunawashukuru sana,” alisema Jaji Mbarouk.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume,
Mheshimiwa Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari, amewahimiza vijana kutumia
mitandao ya kijamii kwa uadilifu, hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Natoa wito kwenu kuwahamasisha vijana
kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuepuka mitandao inayosambaza
habari za chuki na uchochezi,” amesema Jaji Asina.
Ameonya pia dhidi ya matumizi mabaya ya
teknolojia ya akiliunde (AI), ambayo kwa sasa inatumika kusambaza taarifa za
upotoshaji na chuki.
“Vilevile, muwakumbushe vijana wenzenu
kuepuka matumizi mabaya ya akiliunde. Vijana ni kundi lenye nguvu, na mkitambua
nafasi yenu, mtaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha uchaguzi
mkuu wa mwaka huu,” aliongeza.
Katika mikutano yote hiyo, viongozi wa
Tume wamekumbusha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 utafanyika kwa mujibu wa
sheria mbili mpya zilizopitishwa mwaka 2024, ambazo zimeleta maboresho ya
kiutendaji, kisheria na kiuwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk akifungua Mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) uliowakutanisha Tume na wawakilishi wa wanawake kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 jijini Dar es Salaam Julai 31, 2025.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Asina Omari akifungua Mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) uliowakutanisha Tume na wawakilishi wa vijana kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam Julai 31, 2025.
Washiriki katika mkutano huo wa wakilishi wa Vijana wakifuatilia hotuba ya ufunguzi.