Pwani, Julai 31, 2025
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selamani Jafo ameeleza kuwa ,ndani ya muda mfupi, Tanzania haitakuwa na haja ya kuagiza bidhaa mbalimbali za ujenzi kutoka nje ya nchi kama mabati, vioo, nondo, na saruji.
Haya yamebainika Julai 31 ,2025 wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, mkoani Pwani, ambako alizindua Kongani ya Viwanda Kwala pamoja na Bandari Kavu .
“Kwa mfano, mahitaji ya mabati kwa mwaka ni tani 130,000, lakini kwa sasa uzalishaji wa ndani umefikia tani 260,000 kupitia makampuni kama Lodhia, King Lion, ALAF na mengineyo.
“Hii ina maana tuna ziada ya tani 130,000 , hivyo hakuna tena haja ya kuagiza kutoka nje,” alisema Waziri Jafo.
Aliongeza kuwa lengo kuu la serikali ni kupunguza kwa kiwango kikubwa uingizaji wa bidhaa kutoka nje na badala yake kuongeza uzalishaji wa ndani na kusafirisha bidhaa nje ya nchi, hatua itakayosaidia taifa kuingiza fedha za kigeni.
Kwa mujibu wa Dkt. Jafo, kongani ya viwanda Kwala ina jumla ya zaidi ya hekta 1,000 na inatarajiwa kuwa na viwanda zaidi ya 200, huku uwekezaji wake ukikadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 3 za Kimarekani.
Inatarajiwa kwamba bidhaa zitakazozalishwa kwa mwaka zitakuwa na thamani ya hadi dola bilioni 6, ambapo bilioni 2 zitatokana na mauzo ya nje na bilioni 4 kwa matumizi ya ndani.
“Wizara yangu itasimamia kwa karibu maono ya Mhe. Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano katika sekta ya viwanda , tukizalisha zaidi kwa ajili ya soko la ndani na la nje,” alisisitiza.