Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) yaliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga yameshauriwa kuongeza juhudi katika kuchochea maendeleo ya jamii badala ya kusubiri utekelezaji kutoka kwa Serikali pekee.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Nyakia Ally Chirukile wakati akifungua Kongamano la Mashirika yasiyo ya Kiserikali lililowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mafanikio ya sekta hiyo katika nyanja mbalimbali Nchini.
Mhe. Chirukile amesisitiza kuwa mashirika hayo yanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kuhusu maadili mema, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, uhifadhi wa mazingira pamoja na kuhamasisha usafi wa mazingira ili kuijenga jamii yenye ustawi wa kijamii na kiuchumi.
“NGO’s zina mchango mkubwa katika maendeleo ya na kwa kushirikiana kwa pamoja kutaleta maendeleo kwa taifa.
Ni muhimu ziendelee kushirikiana na Serikali katika kuibua na kutatua changamoto zinazokabili wananchi, ninyi wadau wa maendeleo toeni elimu kwa jamii kuhusu uadilifu na kukemea tabia ovu katika jamii” amesema Mhe. Chirukile.
Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Pendo Mangali amewataka washiriki hao kutoka mashirika mbalimbali kufanya kazi kwa ukaribu na ushirikiano mkubwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wao, baadhi ya wawakilishi wa Mashirika hayo walioshiriki kongamano hilo wamepongeza hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira bora ya Taasisi hizo kufanya kazi mbalimbali za maendeleo kwa usatawi wa Jamii.
Mkutano huo umeimarisha mshikamano kati yao na Serikali huku wakiahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
“Tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kuondokana na changamoto mbalimbali ambazo zinaikabili jamii katika kufanikisha maendeleo”.wamesema