Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Bw. Holle Makungu, akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 1, 2025, jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke inawachunguza watia nia wawili wa nafasi ya ubunge (majina yamehifadhiwa) kwa tuhuma za kushawishi kutoa rushwa kwa wajumbe watakaohusika kupiga kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 1, 2025, jijini Dar es Salaam kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Bw. Holle Makungu, amesema kuwa watuhumiwa wameachiwa kwa dhamana, huku uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo unaendelea katika hatua za awali.
Bw. Makungu amesema kuwa taarifa tayari zimewasilishwa kwa chama husika, ambacho kimechukua hatua ya kutoyarejesha majina ya watuhumiwa hao katika mchakato wa kura za maoni.
Bw. Makungu amewataka wagombea pamoja na wapiga kura kufuata sheria za uchaguzi, huku akieeleza kuwa makosa ya rushwa katika uchaguzi ni pamoja na kununua au kuuza kadi ya mpiga kura kwa lengo la kumzuia mtu kupiga kura, kutoa rushwa kwa mgombea ili amuunge mkono au ajitoe kugombea, kutoa rushwa ili mtu ateuliwe kuwa mgombea.
Katika hatua nyingine, Bw. Makungu amesema kuwa TAKUKURU imefuatilia miradi tisa ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi 7,420,000,049.88 katika sekta za elimu, afya, ujenzi, na biashara.
Amesema kuwa kati ya miradi hiyo, miradi mitatu ilibainika kuwa na dosari mbalimbali ambapo ushauri ulitolewa kwa ajili ya marekebisho.
“Ushauri huo ulitekelezwa na Wakurugenzi wa Manispaa za Temeke na Kigamboni ambao ndiyo wasimamizi wa miradi hiyo,” amesema Bw. Makungu.
Kupitia programu ya TAKUKURU Rafiki, amesema kuwa taasisi hiyo imetoa elimu katika kata nane na kuibua jumla ya kero 70 kutoka sekta mbalimbali zikiwemo barabara, elimu, na ujenzi ambapo kati ya hizo, kero 65 zimetatuliwa kwa kushirikiana na wadau husika, huku tano zikiendelea kufanyiwa kazi.
Ametoa mfano wa changamoto zilizobainika, ikiwemo Soko la Mbagala Kizuiani ambalo halina miundombinu bora.
“Wananchi wameomba soko hilo liboreshwe, na tayari maboresho yanaendelea kuanzia katika eneo la wauza samaki, aidha, wafanyabiashara wa Soko la TAZARA wameomba kukamilishwa kwa ujenzi wa vyoo vipya, na kazi hiyo inaendelea,” amesema.
Bw. Makungu ameongeza kuwa TAKUKURU imepokea malalamiko 58, ambapo 40 yalihusu rushwa na 18 hayakuhusu rushwa, huku Kesi mbili zimefunguliwa mahakamani, na hivyo kufanya jumla ya kesi 13 zinazoshughulikiwa na mahakama kwa sasa.
Kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, TAKUKURU Mkoa wa Temeke imepanga kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, sambamba na kuhimiza wananchi kuepuka kushiriki vitendo vya rushwa.
“Natoa wito kwa wananchi wote kuepuka kushiriki katika vitendo vya rushwa, na kutoa taarifa wanapobaini viashiria vyake kwa kuwasiliana na Ofisi ya TAKUKURU iliyo karibu nao au kwa kupiga simu bure namba113,” amesema.