Na. Peter Haule na Saidina Msangi ,WF, Dodoma
Msimamizi wa Kitengo cha Maktaba, Wizara ya Fedha, Bi. Pendo Kavalambi, amesema kuwa Mfumo wa Hazina ya Machapisho (Mof respository) umekuwa nyenzo muhimu kwa wananchi wakiwemo wanaofanya tafitini kuhusu masuala ya uchumi na fedha.
Amesema hayo jijini Dodoma wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.
Bi. Kavalambi alisema kuwa Mfumo huo ambao unapatikana kirahisi kwa njia ya Simu janja na vifaa vingine vya kielektroniki kama kompyuta unamuwezesha mtumiaji kupakua taarifa za hali ya uchumi, deni la Taifa, Sheria ya Fedha na Bajeti Kuu ya Serikali tangu uhuru.
Alisema machapisho hayo yanasaidia kuongeza ufahamu wa masuala ya uchumi na kuwasaidia vijana kufahamu juhudi zilizofanywa na Serikali katika kupiga hatua za maendeleo tangu kupatikana kwa uhuru.
Bi. Kavalambi alisema kizazi cha sasa hakina taarifa ya kutosha kuhusu mwenendo wa uchumi tangu uhuru, hivyo kupitia Mfumo huo ni wazi kwamba vijana wanaweza kuwa na hoja za msingi wanapo fuatilia maendeleo ya kiuchumi na hatua ambayo Tanzania imepiga ukilinganisha na nchi nyingine hususani za Afrika.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kutembelea Banda la Wizara ya Fedha katika maonesho hayo ili kupata taarifa za kina kuhusu mfumo huo.
Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) kwa mwaka 2025 yalizinduliwa rasmi Agosti 1, 2025 katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma na Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 8, 2025.




Afisa Mwandamizi kutoka Idara ya Usimamizi wa Bajeti, Wizara ya Fedha, Bw. Boniface Kilindimo, akitoa elimu kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali kwa wakazi wa Dodoma walipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)