

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia Timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi ya ufunguzi ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024), ambapo Tanzania itapambana na Burkina Faso.
Rais Samia ametoa kauli hiyo Agosti 1, 2025, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam, na kubainisha kuwa ana imani kubwa na kikosi cha Taifa Stars, huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa nguvu timu yao.
“Watanzania tuna imani kubwa na wachezaji wetu, na kama kombe litabaki nyumbani, wajue wana tuzo yao kutoka kwangu,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amewahimiza Watanzania kuwakaribisha kwa ukarimu wageni wote wanaofika nchini kushiriki katika mashindano hayo ya kimataifa. Ametoa rai ya kuzingatia utulivu, heshima, ukarimu na amani, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi salama na yenye upendo.
Mashindano ya CHAN 2024 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi leo, Agosti 2, 2025, na Tanzania ikiwa mwenyeji, macho ya Afrika yatakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo historia mpya ya soka la nyumbani inaanza kuandikwa.