
Sista Francis Piscatella, raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 112, ametambuliwa rasmi na Guinness World Records kama mtawa mzee zaidi duniani.
Sista Francis alizaliwa mwaka 1913, na ametumikia Kanisa Katoliki kwa miaka 94, akishuhudia matukio makubwa ya kihistoria kama vita viwili vya dunia, utawala wa Marais 20 wa Marekani, na huduma ya Mapapa saba tofauti.
Alijiunga na nyumba ya watawa mwaka 1931, na baadaye akawa mwalimu wa hisabati, akihudumu katika shule na vyuo vikuu hadi alipofikisha umri wa miaka 84. Ana shahada ya kwanza na ya uzamili, ishara ya bidii yake katika elimu na huduma ya kiroho.
Kwa sasa, Sista Francis anaishi Lancaster, Marekani, ambapo licha ya kutumia kiti cha magurudumu na kuwa kiziwi kiasi, bado ana akili timamu na ni mtu wa bidii ya kiroho anayeendelea kuhamasisha na kuelimisha kwa hekima yake ya miaka mingi.