Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akimsikiliza Mtaalamu wa Nishati kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ya Zambia Fabrizio Marino aliyefika katika banda la taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka kwa ajili ya kufahamu huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa. JKCI inashiriki katika maonesho hayo kwa kutangaza huduma za matibabu ya moyo inazozitoa, kutoa elimu na ushauri wa magonjwa ya moyo na kupima vipimo vya awali vya magonjwa ya moyo.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akimkabidhi zawadi Waziri wa Fedha na Mipango wa Zambia Mhe. Dkt. Situmbeko Musokotwane alipotembelea banda la taasisi hiyo lililopo katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akimweleza Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Dkt. Mpoki Ulisubisya huduma zinazotolewa na taasisi hiyo katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka. (Picha na JKCI)
………….
Na Mwandishi Maalumu – Lusaka, Zambia
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati ya kutoa huduma bora za matibabu ya moyo katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa kushiriki katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara yanayofanyika jijini Lusaka, Zambia.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika banda la taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Alex Joseph alisema ushiriki wa taasisi hiyo katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kupeleka elimu, huduma za uchunguzi, na ushauri wa kiafya kwa wananchi wa Zambia na nchi jirani.
Dkt. Alex alisema taasisi hiyo imekwenda Zambia siyo kwa ajili ya kutangaza huduma peke yake bali pia kushirikiana na Hospitali ya Moyo ya Zambia katika mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo.
“Tumeleta timu ya madaktari bingwa kwa watoto na watu wazima kwa ajili ya kutoa huduma ya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, ushauri wa kitaalamu na kutoa elimu ya afya ya moyo”.
“Wananchi wengi waliotembelea katika banda letu wamepata elimu ya magonjwa ya moyo, kuna ambao tumewafanyia vipimo vya awali vya moyo ambavyo ni shinikizo la damu na wingi wa sukari kwenye damu huku wengine wakihamasika kujifunza kuhusu njia za kujikinga dhidi ya magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Alex.
Dkt. Alex alisema JKCI pamoja na kutoa huduma za kawaida pia inatoa huduma za matibabu katika kliniki maalum (VIP Clinic) kwa wagonjwa wa ndani ya nchi na International Clinic kwa wagonjwa wanaotoka nje ya Tanzania.
“Tunazo huduma za VIP Clinic kwa wale wanaohitaji huduma za haraka vilevile International Clinic kwa wageni kutoka nje ya nchi. Huduma hizi zimeongeza ufanisi wa upatikanaji wa tiba ya moyo kwa watu wa mataifa mbalimbali, ikiwemo Zambia”, alifafanua Dkt. Alex.
Baadhi ya wananchi wa Zambia waliopata huduma katika banda hilo waliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kujali maisha ya watu bila ya kuangalia mipaka ya kitaifa iliyopo.
“Nimefurahishwa sana na huduma niliyoipata kutoka kwa madaktari wa Tanzania, ni ya kitaalamu, ya haraka na yenye huruma, nimepewa ushauri muhimu kuhusu namna ya kuishi maisha yenye afya ya moyo. Nashukuru sana JKCI kwa kufika hapa Zambia”, alishukuru Joseph Banda mkazi wa Lusaka.
Naye Mary Tembo, mama wa mtoto aliyefanyiwa uchunguzi wa moyo alisema mtoto wake alikuwa analalamika maumivu ya kifua mara kwa mara baada ya kufika katika banda hilo wamepata huduma bila malipo kutoka kwa madaktari wa Tanzania, aliishukuru JKCI kwa moyo wa ubinadamu walionao.
Kwa upande mwingine JKCI imetumia maonesho hayo kama jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa afya baina ya Tanzania na Zambia, sambamba na kuonesha uwezo wa wataalamu wake katika kutoa huduma za kibingwa bobezi ambazo zimeendelea kuokoa maisha ya maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya Tanzania.