Na Mwandishi wetu.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Abdul-razaq Badru ametembea kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni Mkoani Tanga kujionea uendelezaji wa eneo hilo ambalo linatumika kwa ajili ya kuwamishia wananchi tarafa ya Ngorongoro wanaojiandikisha kuhama kwa hiari.
Akiwa na mwenyeji wake mkuu wa wilaya ya Handeni mhe. Salum Nyamwese,kamishna Badru amesema mamlaka itashirikiana na wizara za kisekta katika kuhakikisha kijiji hicho kinaendelea kuwa cha mfano kwa kukiwekea miundombinu yote wezeshi kwa ajili ya wananchi wanaohamia.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya kuna kazi kubwa ambayo serikali imefanya, tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha kijiji hiki kinakuwa bora ili wananchi waliohamia na wale watakaohamia waweze kuishi hapa kwa furaha,”alisema Kamishna Badru.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Handeni mhe. Nyamwese alisema kuwa kazi mbalimbali za uboreshaji wa miundo mbinu katika kijiji hicho zinaendelea ikiwa sambamba na ulinzi wa Nyumba ambazo zimeshakamilishwa kujengwa.
Kijiji cha Msomera kimekuwa ni cha mfano kutokana na serikali ya awamu ya sita kuamua kuweka miundombinu yote ya msingi ili wananchi wanaoishi eneo la Ngorongoro waweze kuhamia kupisha shughuli za uhifadhi katika hifadhi hiyo.