Na Silivia Amandius Bukoba
Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imejipambanua katika maonyesho ya Nane Nane mwaka 2025 kwa kutoa elimu ya kina kuhusu teknolojia za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi, sambamba na kuhamasisha lishe bora kwa wananchi.
Maonyesho hayo yanafanyika kwa siku kumi katika Viwanja vya Kayakailabwa, kuanzia Agosti 1 hadi 10, 2025, na yamekuwa kivutio kikubwa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa.
Akizungumza katika banda la maonyesho hilo, Afisa Mifugo wa Halmashauri hiyo, Bw. Bucha Kundi, alisema wananchi wanapata nafasi ya kujifunza mbinu bora za kilimo na ufugaji wa kisasa, uvuvi, pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu lishe.
“Tunatoa elimu ya kilimo cha kisasa, ufugaji bora, pamoja na uvuvi. Pia tunawashauri wakulima kuhusu afya ya udongo kwa kuwasaidia kupima udongo ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wao,” alisema Bw. Kundi.
Banda hilo pia limesheheni bidhaa na mazao mbalimbali ikiwemo mboga mboga, matunda, mazao ya nyuki, mifugo na mazao ya shambani. Mashamba darasa ya mboga, kahawa, migomba, matunda, mpunga na bwawa la samaki yamekuwa kivutio kikuu kwa wageni.
Aidha, shughuli za lishe zimepewa kipaumbele kwa kutoa huduma za upimaji wa uzito, presha na ushauri wa lishe bora kwa lengo la kupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuhamasisha afya njema.
Maonyesho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kauli mbiu:
“Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.”