Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema jeshi hilo linatekeleza kikamilifu maelekezo ya viongozi wa kitaifa ikiwemo ya kutakiwa kuendelea kuonesha shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi zinazofanywa na JKT hata baada ya maonesho ya wakulima (Nanenane) kuhitimishwa Agosti 8, 2025.
Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo leo Agosti 4, 2025 alipotembelea eneo la JKT katika viwanja vya maonesho ya Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesema JKT imejenga miundombinu ya kudumu kwenye eneo lao, hivyo wapo katika eneo hilo mwaka mzima, sio wakati wa maonesho ya Nanenane pekee.
Mkuu huyo wa JKT ambaye ametembelea maeneo mbalimbali kama eneo la mifugo, mabwawa ya samaki, vipando (mashamba darasa) pamoja na zana na teknolojia za kilimo, amewahimiza Watanzania kutembelea eneo la JKT na maonesho ya Nanenane kwa ujumla ikiwemo katika mabanda ya jeshi hilo katika maonesho yanayoendelea katika kanda mbalimbali nchini ili kupata elimu ya namna jeshi hilo limejikita katika kilimo.