WAKALA wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) unashiriki katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Ushiriki wa PBPA katika maonesho haya unalenga kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya msingi, ambayo ni pamoja na usajili wa wazabuni na kampuni za uagizaji mafuta, usimamizi wa mikataba ya uagizaji mafuta, usimamizi wa huduma za upakuaji mafuta, pamoja na uratibu wa mahitaji ya bidhaa za mafuta kwa ajili ya matumizi ya ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza katika banda la PBPA Mhandisi Prudence Laurian amesema kuwa ushiriki wa wakala huo unatoa fursa kwa wananchi kuelewa kwa undani kuhusu Mfumo Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System), manufaa yake kwa taifa, na mchango wa PBPA katika kulinda usalama wa nishati ya mafuta nchini.
“Tunatumia jukwaa hili kueleza wadau namna tunavyoratibu ununuzi wa mafuta kwa pamoja, faida zinazopatikana zikiwemo kupunguza gharama, kuimarisha upatikanaji wa mafuta, na kuhakikisha sekta ya usafirishaji, kilimo, viwanda na huduma nyingine zinapata mafuta kwa wakati,” amesema Mhandisi Prudence.
Aidha, PBPA imeendelea kuweka msisitizo katika kuelimisha wananchi kuhusu hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuhakikisha usalama wa mafuta nchini, ikiwa ni pamoja na kudhibiti upotevu wa bidhaa hizo muhimu.
Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio ya sekta ya kilimo na wadau wake, huku yakitoa fursa kwa taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi, na wananchi kushirikiana katika kuendeleza kilimo na uzalishaji nchini. Kwa PBPA, maonesho haya ni njia mojawapo ya kuonesha namna nishati ya mafuta inavyokuwa sehemu ya mnyororo wa maendeleo ya kilimo.
Maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 8 Agosti 2025, yakihudhuriwa na wadau wa kilimo Wizara, taasisi za elimu na utafiti, pamoja na mashirika ya umma na binafsi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.