WANAWAKE wamehimizwa kujiunga kwenye Vyama vya Ushirika ili waweze kujikomboa kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zilizopo kwenye Ushirika ikiwemo urahisi wa upatikanaji wa masoko, pembejeo za Kilimo na urahisi wa upatikanaji wa mitaji kupitia Mikopo ya riba nafuu kwenye Vyama vya Ushirika.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa COPRA na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ushirika, Irene Madeje, wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la pili la Wanawake wanaushirika lililofanyika leo Agosti 04, 2015 katika Viwanja vya Nanenane Jijini Dodoma.
Amesema kwenye Ushirika ndio sehemu pekee inayoweza kuwatoa wanawake kwenye changamoto zinazokwamisha kupiga hatua za kimaendeleo hivyo wanawake watumie fursa zilizopo kwenye Ushirika.
Aidha, amewapongeza Wanawake walioshiriki Jukwaa hilo kwa mshikamano katika kusukuma gurudumu la Maendeleo kwenye Sekta ya Ushirika kupitia Vyama vya Ushirika.
“Ushirika ndio nguzo ya Uchumi na sisi wote tunatambua; niwapongeze wanawake wanaushirika kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Ushirika unasonga mbele,” amesema Madeje
Jukwaa hilo limehudhuriwa na Wanawake kutoka kanda Saba (7) za Tanzania Bara na Visiwani ambazo ni kanda ya kaskazini, kusini, Pwani, nyanda za juu kusini, kanda ya Kati, kanda ya ziwa na Zanzibar na linafanyika kwa muda wa siku mbili ambapo litahitimishwa kesho Agosti 5, 2025.