Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Italia kupitia Mradi wa TELMS II, imeazimia kuendeleza mageuzi katika elimu ya ufundi kwa kuziimarisha Taasisi za elimu ya ufundi ili kuchochea maendeleo endelevu nchini.
Kupitia kikao cha kamati ya pamoja leo Agosti 05, 2025 Dkt. Kenneth Hosea, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema kuwa Mradi wa TELMS II unatekelezwa kwa bajeti ya Euro milioni 19.79 (sawa na Sh. Bilioni 54). Fedha hizo ni mkopo nafuu kutoka Serikali ya Italia kwa Serikali ya Tanzania kupitia makubaliano rasmi.
Ameongeza kuwa, Mradi huo wa miaka mitano (2025/2030) utasaidia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo, kwani unalenga kukuza teknolojia, ubunifu na ujasiriamali. Pia uta kuimarisha maendeleo ya nishati endelevu pamoja na suala la uhifadhi mazingira.
Naye Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Giuseppe Sean Coppola, amesema Serikali ya nchi yake inajivunia mahusiano chanya ya kidiplomasia na Tanzania, hasa kupitia ushirikiano katika miradi ya elimu inayolenga kuwajengea Watanzania ujuzi na maarifa kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Mratibu wa Mradi huo, ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Fredrick Salukele amesema kuwa wanufaika wa Mradi wa TELMS II ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST).
Kikao hicho kimehudhuriwa na Makamu Mkuu wa Chuo cha MUST Prof. Aloys Mvuma, Mkuu wa Chuo cha ATC Prof. Prof. Musa Chacha, Mkuu wa Chuo DIT Prof. Preksedis Ndomba pamoja na
Mkuu wa Taasisi ya KIST Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi.