Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Dkt. Cosmas Mwaisobwa, Msaidizi wa Makamu wa Rais (Hotuba) akipokea Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Presscard) kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) Wakili Patrick Kipangula.
Dkt. Mwaisobwa amepokea Kitambulisho hicho tarehe 05 Agosti, 2025 katika Ofisi za Bodi zilizopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam, baada ya kukidhi vigezo vinavyohitajika Kisheria akiwa na Elimu ya juu iliyotajwa katika Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ya Daktari wa Falsafa ya Mawasiliano kwa Umma.
Mwaisobwa ni miongoni mwa Wataalamu wachache nchini wenye Elimu ya Udaktari wa Falsafa ya Mawasiliano kwa Umma na Uandishi wa Habari waliopewa vitambulisho, akitanguliwa na Dkt. Egbert Mkoko (Mjumbe wa Bodi) na Dkt. Ayoub Chacha Rioba (Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania TBC).
Akizungumza mara baada ya kumkabidhi kitambulisho hicho, Wakili Kipangula amempongeza Dkt. Mwaisobwa kwa kutekeleza takwa la Kisheria na kuwasihi waandishi wengine ambao bado hawajajisajili kuhakikisha wanafanya hivyo ili waweze kuendelea kutekeleza majukumu yako ya kihabari bila kukinzana na Sheria.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari-JAB imepokea maombi zaidi ya 3,200 kwa ajili ya Ithibati na Vitambulisho vya Uandishi wa Habari na tayari maombi 2,109 yameidhinishwa hadi kufikia tarehe 5 Agosti, 2025 huku maombi 43 kati ya hayo yakikataliwa kutokana na kutokidhi vigezo na 674 yakiwa katika mchakato wa kuthibitishwa.