Mwanasheria wa TIRA, Bw. Okaka Jairo akizungumza na Fullshangwe katika maoenesho ya Nanenane mkoani Dodoma.
Msajili wa Migogoro katika Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima, Bw. Jamali Mwasha.
…………
Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshiriki katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma, kwa lengo la kutoa elimu juu ya umuhimu wa bima katika sekta ya kilimo, ufugaji, na uvuvi.
Akizungumza katika banda la Mamlaka hiyo, Mwanasheria wa TIRA, Bw. Okaka Jairo, alisema ushiriki wao kwenye maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha wananchi kutambua faida za bima, hususan kwa wakulima na wafugaji wanaokumbwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi kutokana na majanga ya asili.
“Katika shughuli hizi za Nanenane, tunatoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bima inaweza kuwasaidia kukabiliana na majanga kama ukame, mafuriko, magonjwa ya mifugo, na uharibifu wa mazao. Elimu hii ni muhimu kwa kuongeza usalama wa kipato na mali zao,” alisema Bw. Jairo.
Alisema kuwa TIRA imekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya bima wakiwemo watoa huduma wa bima binafsi, Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania, pamoja na washauri wa bima za kilimo. Kikao hicho kilijumuisha kampuni 15 zinazotoa bidhaa za bima ya kilimo.
“Vilevile tulikuwa na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania ambao walizungumza kuhusu umuhimu wa bima katika shughuli za bandari, hususan kwa bidhaa zinazoingia nchini ambazo kisheria zinapaswa kuwa na bima kutoka kampuni zilizosajiliwa nchini,” aliongeza.
Bw. Jairo alibainisha kuwa huduma za bima haziwezi kutolewa kwa mafanikio na mdau mmoja peke yake, bali zinahitaji ushirikiano wa wadau wote, jambo lililowapelekea kushiriki kwa pamoja katika banda moja ili kuelimisha wananchi.
Katika kikao hicho, wadau waligusia bidhaa mbalimbali za bima ya kilimo, hasa zinazolenga maeneo ya uzalishaji, ufugaji, na uvuvi, pamoja na umuhimu wa bima kwa mtu mmoja mmoja katika kulinda shughuli zake dhidi ya hasara zisizotarajiwa.
Naye Msajili wa Migogoro katika Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima, Bw. Jamali Mwasha, alisema kuwa bima ya kilimo ni nyenzo muhimu ya kumwezesha mkulima kukopesheka kwa urahisi, kwani hutoa uhakika wa fidia pindi janga linapotokea.
“Mkulima akipata hasara kutokana na ukame au wadudu waharibifu, kama hana bima atapoteza kila kitu. Lakini akiwa na bima, atalipwa fidia, ataweza kuendelea na shughuli zake na hata kukuza biashara yake,” alisema Bw. Mwasha.
Alisisitiza kuwa bima ni chombo muhimu cha ustawi wa uchumi na inaweza kuwa kichocheo cha kuongeza uzalishaji na usalama wa kipato kwa wakulima, wafugaji, na wavuvi nchini.