#Aipongeza TARURA kuendelea kufungua barabara vijijini
Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa kutoka OR-TAMISEMI Bi. Beatrice Kimoleta amewataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi wa mitaro ya maji kuzunguka maeneo yao.
Bi. Kilemeta ameyasema hayo alipotembelea banda la Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwenye Maonesho ya NaneNane Kitaifa kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema kwamba wapo baadhi ya wananchi hawasafishi mitaro ya maji kwenye barabara zinazopita kwenye nyumba zao na hivyo maeneo yao kuwa machafu wakati wote.
“TARURA endeleeni kutoa elimu kwa wananchi wasafishe mitaro inayopita kwenye nyumba zao,ipo mitaa unakuta kuna barabara nzuri za lami lakini kuna nyasi nyingi na wengine wana magenge mbele ila uchafu wote wanatupa kwenye mitaro hiyo na hawasafishi”.
Ameongeza kusema kwamba wananchi wakijenga utamaduni wa kusafisha na kulinda miundombinu ya barabara inayowazunguka, itadumu kwa muda mrefu.
Aidha, amewapongeza TARURA kwa kazi nzuri wanayoifanya nchini kwa kuwafungulia barabara wananchi na hivyo kuwarahisha mawasiliano katika maeneo mengi.
Naye, Bw. Frank Urio Mkazi wa kijiji cha Kimangaro, Kata ya Mwika Kusini Wilaya ya Moshi vijijini ameipongeza TARURA kwa kuwawezesha kujenga barabara katika kijiji chao Kwa gharama zao kupitia michango ambapo TARURA imewasaidia ushauri wa kitaalamu ikiwemo vipimo stahiki vinavyotumika katika ujenzi wa barabara hasa za vijijini.
Amesema kutokana na kujitolea kwao TARURA imeweza kuipa kipaumbele barabara hizo kwa kutoa wataalam wao kusimamia ujenzi wa barabara hizo , kukubali kujenga makalavati ili maji yasiharibu barabara hizo pamoja na kuweka changarawe na hivyo kusaidia nguvu za wananchi.
Hata hivyo Bw. Urio ametoa wito wa wananchi wa Kimangaro, Kiruweli na vijiji vingine waliojitolea na kufaidika na barabara hizo wazitunze na kuhakikisha zinakuwa katika hali ya usafi, kutokutupa takataka na hawaharibu alama za barabarani ili zidumu kwa muda mrefu.