Na John Bukuku – Nane Nane, Dodoma
Meneja Masoko wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Maiko Mwanachuo, amesema kuwa shirika hilo lina mchango mkubwa kwa wakulima na wauzaji nchini kwa kusafirisha pembejeo na bidhaa mbalimbali kwa gharama nafuu.
Akizungumza leo Agosti 5, 2025, na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Bw. Mwanachuo alisema kuwa Posta inawaunganisha wakulima, wazalishaji na wanunuzi kwa kuwasafirisha bidhaa kutoka kwa wauzaji hadi kwa wakulima.
“Shirika la Posta linasafirisha mbegu na pembejeo kutoka kwa wauzaji hadi kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini. Hii ni sehemu ya dhamira yetu kusaidia maendeleo ya kilimo na kuwa kiungo muhimu kati ya wazalishaji na walaji,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa katika maonesho ya mwaka huu, shirika hilo linatoa huduma ya kusafirisha mizigo ya wateja kutoka viwanjani hadi majumbani kwa kutumia bajaji maalum kwa bei nafuu, huduma ambayo imepokelewa vizuri na wananchi.
Kwa mujibu wa Bw. Mwanachuo, huduma nyingine zinazotolewa kwenye banda la Posta ni pamoja na usajili wa huduma ya EMS, ufunguaji wa sanduku la barua pamoja na ulipaji wa ada za masanduku hayo.
“Kwa wale wanaohitaji kujisajili kwa huduma mbalimbali kama vile VICHO BOX, wanaweza kufika moja kwa moja kwenye banda letu na kupata huduma hizo kwa urahisi,” aliongeza.
Bw. Mwanachuo alitoa wito kwa wananchi wanaotembelea maonesho ya Nane Nane kufika katika banda la Posta ili kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo la umma.