Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Nchi Zisizo na Mlango wa Bahari (Bandari) ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godious Kyaharara anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo unaofanyika Awaza, nchini Turkmenistan tarehe 5–8 Agosti, 2025.
Akifungua Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Turkmenstan Mheshimiwa Serdar Berdimuhamedow amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, hasa ushirikiano wa nchi za Kusini Kusini katika kukabiliana na changamoto za kipekee zinazozikabili nchi zisizo na bahari na kutoa wito wa ushirikishwaji jumuishi unaohusisha Serikali, mabunge, vijana, na asasi za kiraia.
Rais alithibitisha msimamo wa Turkmenistan wa kutokuegemea upande wowote na kueleleza kuunga mkono utekelezaji wa Mpango wa maendeleo wa miaka 10 ijayo wenye lengo la kukuza miunganisho, ustahimilivu na maendeleo endelevu kwa nchi zisizo na bahari.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Mhe. António Guterres, alisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa wenye nguvu na wa vitendo ni muhimu zaidi kwa wakati huu kwa kuwa changamoto za dunia kama za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kiuchumi, na miundombinu hafifu zinahitaji majibu ya pamoja, hasa kwa nchi zisizo na bahari.
Alitoa wito wa kuwekeza katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2024–2034 na kuongeza kuwa Diplomasia ya usafirishaji ni kiungo muhimu katika kufungua mustakabali wa biashara kwa nchi za zisizo na bahari ili kuendeleza maendeleo jumuishi kwa kuwa maendeleo ya nchi hizo ni mafanikio ya dunia nzima na kwamba ustahimilivu wa kijamii na kiuchumi unaweza kufikiwa tu kupitia mikakati inayojumuisha kila mwananchi wa nchi hizo.
Mkutano huo umeandaliwa na Umoja wa Mataifa, kwa kushirikiana na Serikali ya Turkmenistan unalenga kutathmini utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Vienna kwa Nchi Zisizo na Mlango wa Bahari wa Mpango kazi wa Vienna wa 2014–2024 na kuweka ajenda mpya ya maendeleo jumuishi kwa kipindi cha miaka kumi ijayo.
Mkutano huo unawakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi, na wadau wengine kujadili changamoto na fursa zinazozikabili nchi zisizo na bahari ambazo hukabiliwa na gharama kubwa za usafirishaji, utegemezi wa nchi jirani kufikia masoko ya kimataifa, pamoja na changamoto za miundombinu na usafirishaji wa bidhaa.
Mkutano huo pia utajadili mafanikio, changamoto na kujifunza kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Vienna na Kuandaa mpango mpya wa miaka 10 – Utakaowezesha nchi hizi kuongeza ushindani wa kiuchumi, kuimarisha miundombinu ya usafiri, kuongeza ushiriki wa biashara ya kikanda na kimataifa.
Malengo mengine ni Kukuza ushirikiano wa kimataifa – Kati ya LLDCs na washirika wa maendeleo, nchi za mpakani, mashirika ya kikanda na sekta binafsi, Kuweka msisitizo kwa maendeleo ya kidigitali na teknolojia – Kama njia mbadala ya kupunguza utegemezi wa kimwili kwenye masoko ya nje.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa Tamko la Kisiasa la Awaza na mpango kazi mpya wa kimataifa wa miaka 10 kwa Nchi zisizo na Bandari utakaolenga kuboresha muunganiko wa miundombinu kati ya nchi zisizo na bandari na zile zenye bandari, Kuweka mazingira wezeshi kwa biashara, uwekezaji, na huduma za usafirishaji, Kuhimiza matumizi ya teknolojia na dijitali katika kuboresha huduma za mpaka na ufanisi wa biashara na Kuimarisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa vijana na ushirikiano wa sekta binafsi.
Mkutano huo ni jukwaa muhimu la majadiliano ya kimataifa kuhusu maendeleo jumuishi yenye usawa kwa nchi zisizo na mlango wa bahari ambapo ushiriki wa mataifa jirani na Nchi za LLDCs, ni muhimu katika kuhakikisha kuwa maendeleo haya yanakuwa endelevu na ya manufaa kwa wote.
Mkutano huo unaendeshwa chini ya kauli mbiu isemayo “Kufungua Fursa kwa Nchi Zisizo na Bahari kwa Maendeleo Endelevu kupitia Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa”.