Na WAF, Dodoma
Serikali kwa kushirikina na Shirika la Kimataifa la Ujerumani Hellen Keller, imewatibu wagonjwa wa vikope na kutoa tiba ya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa watu wapatao 100,000 katika Halmashauri 64 nchini.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt.Grace Magembe ameyasema hayo Agosti 4, 2025, mara baada ya kukutana ujumbe wa Shirika hilo katika ukumbi wa Mkutano wa Ofisi ya Wizara ya Afya,Mtumba Jijini Dodoma.
Kikao hicho kilichowakutanisha Rais wa Shirika hilo na ujumbe wake pamoja na Wizara ya Afya kilikuwa na majadiliano yaliyolenga kuimarisha ushirikiano zaidi wa kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza na yale yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo afua za lishe.
Dkt. Magembe ameongeza kuwa Huduma za utoaji wa matone ya vitamini A pamoja na utoaji elimu ya masuala ya lishe hasa kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano ambao unafanyika sana mkoa wa Mara unaendelea kwa kushirikiana na shirika la Hellen Keller.
Katika kikao hicho Wizara ya Afya imejadiliana na Shirika hilo jinsi linavyoweza kuongeza utoaji wa huduma za upasuaji wa vikope na mtoto wa jicho kwenye maeneo mengine pamoja na mafunzo kwa watumishi wa sekta ya Afya.
“ Kama Serikali ni muhimu kuwa na uendelevu hivyo tumekubaliana wanapokuja na wataalam wao pia waweze kufundisha wataalam wa ndani ili kuendelea kutoa huduma kama zinavyotolewa na wataalam wa Hellen Keller lakini pia tumejadili namna ya kushirikiana nao kutoa elimu ya lishe kwenye mikoa ambayo inaudumavu,” amesema Dkt. Magembe.
Naye Rais wa Shirika la Hellen Keller Bi. Sarah Bouchie amesema shirika hilo limefikia malengo kutokana na ushirikiano wa karibu wa Serikali na kupongeza hatua iliyofikiwa na Tanzania kwenye kudhibiti magonjwa hayo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kutoa elimu ya masuala ya lishe na kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele, lishe pamoja na yale yasiyoambukiza.