Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Agosti 5, 2025
Katika zoezi la kupiga kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa ubunge wa majimbo tisa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ameongoza kwa kupata kura za ndiyo 12,074 kati ya kura 12,245 zilizopigwa.
Akitangaza matokeo hayo rasmi, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Pwani, David Mramba, alieleza kuwa kura za hapana zilikuwa 171.
Katika Jimbo la Bagamoyo, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum mkoani Pwani, CPA Subira Mgalu, ameongoza kwa kupata kura 3,544 kati ya kura halali 5,335 ambapo jumla ya kura zilizopigwa zilikuwa 5,567, huku 232 zikiwa zimeharibika.
Mgalu alifuatiwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo aliyemaliza muda wake, Muharami Mkenge aliyepata kura 1,574.
Katika Jimbo la Kisarawe, aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Suleiman Jafo, aliongoza kwa kupata kura 4,412, sawa na asilimia 76 dhidi ya wagombea wengine wanne.
Kwa upande wa Kibaha Mjini, Silvestery Koka aliongoza kwa kura 2,824 kati ya kura halali 5,682, huku kura 53 zikiripotiwa kuharibika.
Jimbo la Rufiji, Muhammed Mchengerwa aliongoza kwa kupata kura 8,465 dhidi ya wagombea wenzake watatu.
Katika Jimbo la Mafia, Omary Kipanga ameibuka kidedea kwa kupata kura 1,186, huku katika Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa ameshinda kwa kura 3,247, sawa na asilimia 62.12.
Kwa Jimbo la Kibiti, Amina Mkumba aliibuka kidedea kwa kura 4,712 dhidi ya wagombea wengine wawili.
Mramba anasema jmbo la Mkuranga, Abdallah Ulega alishinda kwa kupata kura 8,490.
Mchakato huu umefuata taratibu zote za ndani ya chama, na matokeo haya yatawasilishwa kwa ngazi ya juu kwa hatua na mchakato wa kichama unaofuata.