KAIMU Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Njombe, Bw. Henry Msambila,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 5,2025 kwenye banda la WMA katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.
WANANCHI mbalimbali wakipataiwa elimu kuhusu vipimo katika banda la WMA katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-Dodoma
KAIMU Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Njombe, Bw. Henry Msambila, amewataka wananchi kutembelea banda la Wakala huo katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma, ili kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 5,2025 kwenye banda la WMA Bw. Msambila, amesema kuwa Wakala wa Vipimo umejipanga kikamilifu kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo vilivyohakikiwa kisheria katika shughuli za biashara na huduma mbalimbali.
“Tunawahimiza wananchi kufika katika banda letu ili wajifunze kuhusu vipimo sahihi, kutambua vipimo batili, na kuelewa haki zao kama walaji. Elimu hii ni muhimu kwa kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi anayepunjwa katika shughuli za kibiashara,” amesema Msambila
Ameeleza kuwa matumizi ya vipimo visivyo sahihi si tu kwamba ni kosa la kisheria, bali pia yanadhoofisha haki ya mlaji na kuathiri maendeleo ya kiuchumi, hususan kwa wakulima na wajasiriamali wadogo wanaotegemea mizani katika kuuza bidhaa zao.
Aidha, Bw. Msambila amebainisha kuwa Wakala wa Vipimo unaendelea na juhudi za kuhamasisha uadilifu katika biashara kupitia udhibiti madhubuti wa vipimo vinavyotumika sokoni, sambamba na kutoa mafunzo ya utambuzi wa alama halali za mizani na taratibu za kuhakiki vifaa hivyo.
Hata hivyo WMA imewaonya vikali mawakala na wafanyabiashara wanaotumia vipimo visivyo sahihi kuwahadaa wakulima na wananchi, ikisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Wakala wa Vipimo tunaongozwa na Sheria ya Vipimo, Sura ya 340. Tukibaini mtu anafanya udanganyifu kwa vipimo – ikiwemo kuwapunja wakulima – hilo ni kosa la jinai. Tutamchukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria hiyo, ambapo faini zinaanzia shilingi laki moja hadi milioni ishirini,” amesema Msambila.
WMA imeendelea kuwa chombo muhimu katika kusimamia usahihi wa vipimo nchini, ikiwa ni nguzo ya uaminifu katika biashara na ulinzi wa haki za walaji, hususan wakulima wanaotegemea mizani kama njia kuu ya kuuza mazao yao.