Ofisa Ustawi wa Jamii wa Chuo cha Uhasibu (TIA)), Kampasi ya Mwanza, Happiness Godfrey (wa pili kutoka kulia), akizungumza na baadhi ya wananchi waliotembelea banda la chuo hicho leo, katika Maonesho ya Wakulima (Nane Nane),Nyamhongolo, jijini Mwanza.
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
CHUO cha Uhasibu Tanzania (TIA) kimeendelea kung’ara kama moja ya taasisi bora za elimu ya juu nchini, kikijipambanua kwa utoaji wa mafunzo bora ya biashara, uhasibu, masoko, usimamizi wa rasilimali watu, na taaluma nyingine zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumza leo katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza, Ofisa Ustawi wa Jamii wa TIA, Happiness Godfrey, amesema ni chuo cha serikali kilichoanzishwa rasmi mwaka 2002 chini ya Wizara ya Fedha, kikijengwa juu ya uzoefu wa zaidi ya miaka 50 ya kutoa elimu ya biashara na fedha nchini.
“Tunajivunia kutoa elimu bora kuanzia Astashahada (Certificate), Stashahada (Diploma), Shahada (Bachelor Degree) hadi Stashahada ya Uzamili (Postgraduate Diploma). TIA imeendelea kuwa chuo kinachotoa wahitimu wanaotegemewa katika sekta mbalimbali za uchumi na maendeleo ya taifa,” alisema Happiness.
Amesema kwa mwaka wa masomo 2025/2026, TIA inatoa kozi kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza ya Uhasibu,Shahada ya Kwanza ya Elimu (Uhasibu na Masomo ya Biashara), Shahada ya Kwanza ya Ununuzi na Usafirishaji wa Mizigo, Shahada ya Kwanza ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Shahada ya Kwanza ya Masoko na Uhusiano wa Umma
Ofisa Ustawi huyo wa Jamii TIA amesema kuwa, programu hizo zinalenga kutoa elimu ya vitendo na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la sasa na baadaye.
Kwa mujibu wa Happiness, dirisha la maombi ya kujiunga na TIA kwa mwaka wa masomo 2025/2026 sasa limefunguliwa rasmi, ambapo wanafunzi wanahimizwa kutuma maombi kupitia mfumo wa mtandaoni (online application) ulioboreshwa kwa urahisi wa matumizi.
“Tunataka kila Mtanzania mwenye sifa apate fursa ya kujiunga. Mfumo wetu wa maombi mtandaoni ni rahisi, wa kisasa, na unamwezesha mwanafunzi kujisajili popote alipo nchini,” amesema.
Akizungumzia kwa nini wanafunzi wajiunge na TIA amesema n kutokana na kutoa kozi zenye viwango vya kitaifa na kimataifa,ina kampasi saba ikiwemo ya Mwanza, mazingira bora ya kujifunzia yenye miundombinu ya kisasa, ushirikiano na taasisi za umma na binafsi kwa mafunzo kwa vitendo, mikopo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo (HESLB), na uwezo wa kulipa ada kwa awamu kulingana na hali ya kiuchumi ya mwanafunzi
Happiness amesema fursa za ziada kwa wanafunzi wa TIA ni pamoja na Bima ya Afya kwa wanafunzi wote, masomo ya ubadilishanaji (Exchange Programmes) katika vyuo vya Ulaya na Asia,matumizi ya bure ya kompyuta katika maabara za kisasa,maktaba ya kisasa yenye vitabu na rasilimali za kidigitali, mafunzo ya ujasiriamali na namna ya kujiajiri,hosteli kwa wanafunzi wanaohitaji malazi na vipindi vya kukuza vipaji kupitia shughuli mbalimbali za michezo na sanaa
Ofisa huyo ametoa rai kwa wahitimu wa shule za sekondari na vyuo vya kati kuchangamkia fursa ya kusoma TIA, huku akisisitiza kuwa chuo hicho ni kiungo muhimu katika kufanikisha ajenda ya maendeleo ya kiuchumi kupitia elimu ya biashara na fedha.