Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bw, Godwin Gondwe na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni, Bi, Anastazia Tutuba wakisikiliza maelezo kuhusu majukumu ya Bodi ya Bima ya Amana walipotembelea banda la DIB katika maonesho ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi (Nanenane) yanayofanyika kitaifa Nzuguni jijini Dodoma.
Meneja wa Huduma za Kisheria Bodi ya Bima ya Amana, Bw. David Njau, akimkabidhi zawadi Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bw. Godwin Gondwe, wakati alipotembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bw. Godwin Gondwe, akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mwandamizi wa Bodi ya Bima ya Amana, Bi. Joyce Shala, katika bada la Bodi ya Bima ya Amana katika maonesho yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bw. Godwin Gondwe, akizungumza jambo wakati alipotembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika Maonesho ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni, Bi. Anastazia Tutuba.
………….
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Bw Godwin Gondwe, ameitaka Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ili wananchi wengi zaidi wawe na imani ya kutumia huduma za kibenki.
Akizungumza wakati alipotembelea banda la DIB katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Bw Gondwe alisema bado kuna uelewa mdogo wa wananchi kuhusu majukumu ya DIB.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya kuelimisha wananchi kuhusu shughuli zenu. Hata hivyo, nawashauri kuongeza jitihada za mawasiliano ya kimkakati kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa katika halmashauri ili wapate mwamko wa kutumia huduma za kibenki wakijua kwamba amana zao zinakingwa,” alisema Mkuu wa Wilaya baada ya kupata maelezo ya majukumu ya DIB.
Bw. Gondwe ambaye alifuatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni, Bi. Anastazia Tutuba, alisema bado wananchi wengi hawaweki fedha zao benki, pengine kutokana na kukosa elimu muhimu inayotolewa na DIB.
Alitoa mfano wa moto uliozuka hivi karibuni katika soko huko Singida kwamba baadhi ya wananchi walikuwa wanalazimisha kuingia kwenye maduka yao wakati moto unalipuka na walizuiwa kwa nguvu.
“Tulipomaliza kuzima moto, baadhi walieleza kwamba walikuwa na pesa zao wamezifukia. Waliporuhusiwa kwenda kufukua walikoficha, wengine walitoa hadi shilingi milioni 20. Hii inaonesha kwamba elimu bado inahitajika ya umuhimu wa kuhifadhi fedha katika benki zetu na kwamba Bodi ya Bima ya Amana inatakiwa kuwafikia wananchi hao na elimu hii.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Bi. Tutuba alishauri DIB kutumia mikutano ya Wakurugenzi na viongozi wa Serikali za itaa kutoa elimu kuhusu taasisi hii na kwamba wao wana nafasi nzuri ya kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Alisema wilayani kwake, wakulima wengi wa dengu wanapata fedha nyingi na wengi hawatumii huduma za kibenki, hivyo elimu hii inaweza kuwapa imani ya kufungua akaunti na kuweka fedha benki wakijua kwamba zinakingwa.
Awali Meneja wa Huduma za Sheria wa DIB, Bw. David Njau na Afisa Mwandamizi wa DIB, Bi. Joyce Shala walimweleza Mkuu wa Wilaya na ujumbe wake majukumu ya DIB na jinsi yanavyohusiana na maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kwamba wakulima ni wadu wakubwa wa mfuko wa Bima ya Amana.
Wajibu mkuu wa DIB ni kukinga amana za wateja wa benki na taasisi za fedha ili endapo benki ikianguka au kufilisika waweze kupatiwa fidia kwa amana zinazokingwa. Aidha, DIB inasimamia Mfuko wa Bima ya Amana ambao unachangiwa na benki na taasisi za fedha zinazopokea amana kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake.
Katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka huu, Bodi ya Bima ya Amana inashiriki kitaifa jijini Dodoma, Zanzibar, na katika kanda za Mashariki mjini Morogoro, Kaskazini jijini Arusha na Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya.