Na John Bukuku – Dar es Salaam
Dirisha la Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2025/2026 limefunguliwa rasmi leo, Agosti 6, 2025, jijini Dar es Salaam, ambapo waandishi bunifu nchini wametakiwa kuanza kuwasilisha miswada yao kwa ajili ya kushindanishwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo mbele ya waandishi wa habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa huu ni wakati muafaka kwa waandishi kuwasilisha kazi zao ili kuchagiza maendeleo ya lugha ya Kiswahili kupitia uandishi bunifu.
“Wakati sasa umefika wa waandishi kuwasilisha kazi zao bunifu ili ziweze kushindaniwa. Nawaomba wadau mjitokeze kwa wingi,” alisema Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda pia alieleza kuwa kabla ya uzinduzi huo, kikao maalum kilifanyika kati ya Wizara na wadau wa uandishi bunifu kwa lengo la kuboresha mchakato wa tuzo hiyo ili iweze kuwa chombo bora zaidi cha kuhamasisha usomaji wa vitabu na kukuza lugha ya Kiswahili nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Prof. Penina Mlama, amesema miswada itakayopelekwa itajumuisha kazi za Riwaya, Ushairi, Hadithi za Watoto na Tamthilia, sawa na ilivyokuwa katika mwaka wa tuzo uliopita wa 2024/2025.
Prof. Mlama amesema kuwa kamati itaanza kupokea miswada kuanzia Agosti 15, 2025 hadi Novemba 30, 2025 na kuwataka waandishi bunifu kote nchini, bila kujali umri wala mahali walipo, kujitokeza kwa wingi.
“Nawakaribisha waandishi wote wa uandishi bunifu popote walipo kuleta miswada yao. Tuna matumaini mwaka huu tutapokea kazi nyingi zaidi,” alisema Prof. Mlama.
Ameongeza kuwa baada ya kupokea miswada, jopo la majaji litapitia kazi hizo na hatimaye hafla ya kutangaza washindi itafanyika Aprili 13, 2026, ikiwa ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, aliwashukuru wadau wote waliotoa mchango wao katika kikao cha maoni kuhusu uboreshaji wa tuzo hiyo na kusisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kuendeleza tasnia ya uandishi bunifu nchini.
Kikao hicho kimehusisha wadau kutoka sekta mbalimbali ya uandishi bunifu waliotoa mapendekezo na maoni yatakayowezesha tuzo hiyo kuwa chombo chenye ushawishi mkubwa katika kukuza fasihi ya Kiswahili