Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema kuwa mfumo wa Jamii Stack ni suluhisho jumuishi la kiteknolojia linalowezesha mifumo mbalimbali ya kidijitali kubadilishana taarifa na kufanya kazi kwa pamoja, hali inayoongeza tija katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo.
Akizungumza katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika Jijini Dodoma, Afisa TEHAMA kutoka Wizara hiyo, Mwakisisa, alisema Jamii Stack ni mkusanyiko wa teknolojia mbalimbali zinazolenga kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
“Ni mfumo unaosaidia mifumo ya serikali na binafsi kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa urahisi. Hii inaleta tija kubwa katika nyanja mbalimbali, hasa kwa wakulima ambao wanapata taarifa kuhusu magonjwa ya mazao, hali ya hewa, na aina ya udongo wanaolima,” alisema Mwakisisa.
Alifafanua kuwa mfumo huo una sehemu kuu tatu muhimu: mazingira wezeshi, miundombinu ya kidijitali ya umma, na mfumo jumuishi wa kubadilishana taarifa.
Katika sehemu hii, Mwakisisa alitaja uwepo wa minara ya mawasiliano, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, na upatikanaji wa nishati kuwa ni vitu vinavyowezesha mifumo ya TEHAMA kufanya kazi kwa ufanisi.
“Ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwenye miradi mikubwa kama Bwawa la Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kidijitali nchini,” alisema.
Pia, alieleza kuwa mazingira wezeshi yanahusisha utungaji wa sera, sheria na miongozo mbalimbali inayosimamia mifumo ya TEHAMA na matumizi yake.
Alisema sehemu hii inahusisha mambo matatu muhimu: Jamii Namba, Jamii Pay, na mfumo wa Jamii Stack wenyewe.
“Jamii Namba ni utambulisho wa kipekee kama NIDA unaomwezesha mtu kujulikana katika mifumo yote ya TEHAMA. Jamii Pay ni mfumo wa malipo unaowezesha mtu kutuma au kupokea fedha kwa njia ya kidijitali,” alieleza.
Sehemu hii ya mwisho ya Jamii Stack inalenga kurahisisha mawasiliano na ubadilishanaji wa taarifa kati ya mifumo ya serikali na sekta binafsi, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akihitimisha, Afisa huyo alisisitiza kuwa kwa wakulima, mfumo huu unasaidia kwa kiasi kikubwa hasa katika upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa, magonjwa ya mazao, na mbinu bora za kilimo, hivyo kuchangia uzalishaji bora na wa tija.