Na Alex Sonna-DODOMA
MAONESHO ya wakulima maarufu kama Nanenane yameendelea kuonyesha matokeo chanya ya mageuzi ya kilimo nchini, huku Serikali ikiahidi kuongeza nguvu katika kuweka mazingira rafiki kwa wakulima ili kuhakikisha Tanzania inabaki kinara wa uzalishaji wa chakula barani Afrika.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, amesema maonesho hayo yamekuwa darasa muhimu kwa wakulima na taasisi mbalimbali kwa kuwa yanaonesha teknolojia za kisasa, vifaa vya kuongeza tija na bidhaa za kilimo zenye ubora wa kimataifa.
Amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi za umma na binafsi zinazoshiriki katika maonesho hayo na itaendelea kushirikiana nazo kuboresha upatikanaji wa pembejeo bora, masoko ya uhakika na mbinu za uzalishaji zinazolingana na mahitaji ya soko la dunia.
“Tumepiga hatua kubwa bidhaa tulizokuwa tunaziona tu kutoka nje sasa zinazalishwa ndani ya nchi.
Hii ni ishara ya mafanikio makubwa na uthibitisho kuwa Tanzania inaweza kushindana kimataifa katika kilimo na biashara ya chakula,”amesema Dkt. Serera.
Dkt. Serera,ameongeza kuwa maonesho ya Nanenane yameongeza ari na hamasa kwa wakulima wanaohudhuria, wengi wakionesha dhamira ya kutumia mbolea na teknolojia mpya ili kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.
Ameeleza kuwa jitihada za pamoja za Serikali, sekta binafsi na wakulima zimechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula, hatua inayowezesha nchi kusafirisha mazao yake katika nchi jirani na masoko ya kimataifa.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa maonesho hayo, Dkt. Serera amesema kuwa Nanenane ni jukwaa la mafunzo linalowawezesha wakulima kujifunza mbinu bora, kushirikiana na wataalamu na wadau wa kilimo, na kupata suluhisho la changamoto wanazokutana nazo shambani.
Amewataka Watanzania kutumia kikamilifu fursa ya Nanenane kwa kushiriki, kujifunza na kuwekeza katika kilimo cha kisasa ili kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na uhakika wa chakula na linakuwa miongoni mwa vinara wa kilimo Afrika na duniani.







