Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Samwel Sumba, akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 6,2025 mara baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Banda la Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS)
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI imetangaza mpango wa kutenga zaidi ya shilingi bilioni 277 kila mwaka kwa ajili ya kugharamia huduma mbalimbali zinazohusiana na Virusi vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI, ikiwa ni hatua ya kupunguza utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili wa kimataifa.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 6, 2025, na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Samwel Sumba,wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Dkt. Sumba amesema kuwa uwekezaji huo wa fedha kutoka vyanzo vya ndani unaonesha dhamira ya dhati ya serikali katika kuimarisha afua za VVU na UKIMWI, ikiwa ni pamoja na kinga, matibabu, huduma za matunzo na uelimishaji kwa jamii.
“Ni muhimu kwa nchi kuanza kujitegemea kifedha katika mapambano dhidi ya Ukimwi. Hii itahakikisha kuwa huduma za afya zinazohusiana na VVU zinaendelea kupatikana kwa uhakika na kwa wakati, hata kama misaada kutoka kwa wafadhili itapungua au kusimama,” amesema Dkt. Sumba.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Athari za UKIMWI wa mwaka 2022/2023, inakadiriwa kuwa Watanzania kati ya 1,540,000 hadi 1,700,000 wanaishi na virusi vya Ukimwi. Kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi kimefikia asilimia 4.4, ambapo wanawake wanaathirika zaidi kwa asilimia 5.6, ikilinganishwa na wanaume wenye asilimia 3.0.
Pamoja na hali hiyo, Dkt. Sumba amesema kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyopita, hususan katika kupunguza maambukizi mapya, vifo vinavyotokana na Ukimwi, na hali ya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU.
“Iwapo tutalinganisha hali ya sasa na miaka ya 2000, tumeona kupungua kwa kiwango cha maambukizi, vifo na unyanyapaa. Hili ni jambo la kupongezwa,” amesisitiza Dkt. Sumba.
“Iwapo tutalinganisha hali ya sasa na miaka ya 2000, tumeona kupungua kwa kiwango cha maambukizi, vifo na unyanyapaa. Hili ni jambo la kupongezwa,” amesisitiza .
Hata hivyo Dkt.Sumba,ametoa rai kwa wananchi kutambua kuwa janga la Ukimwi bado lipo. Tuchukue hatua: tupime afya zetu, tuanze tiba mapema na tuendelee kufuata masharti ya matibabu kwa ustawi wa jamii yetu,”
Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu si tu kwa sekta ya kilimo na mifugo, bali pia kwa taasisi mbalimbali zinazohusika na maendeleo ya kijamii na afya. Kupitia mabanda ya taasisi kama TACAIDS, wananchi wamepata nafasi ya kujifunza kuhusu afya ya jamii, kinga dhidi ya magonjwa, pamoja na huduma zinazotolewa kwa watu wanaoishi na VVU.