Na Baltazar Mashaka, Mwanza
BODI ya Pamba Tanzania (TCB) imeendelea kuwa kivutio kikubwa katika Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza, kwa kutoa elimu na kusambaza maarifa ya kilimo bora cha pamba kwa wakulima na wadau wengine wa sekta hiyo.
Banda la TCB limekuwa likitembelewa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wakiwemo wakulima, wanafunzi, watafiti, wajasiriamali, na hata wageni wa kimataifa, jambo linaloashiria hamasa na umuhimu wa sekta ya pamba katika maendeleo ya kilimo na uchumi wa taifa.
Akizungumza LEO na waandishi wa habari, Ofisa Kilimo wa Bodi ya Pamba Tanzania, Sharifa Salum, amesema bodi hiyo imeleta teknolojia na imejipanga kikamilifu kutumia maonesho hayo kufikisha elimu sahihi kwa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa, mbolea, viuadudu, pembejeo bora na kanuni za kisasa za kilimo cha pamba.
“Lengo letu ni kuwawezesha wakulima kuongeza tija kwa kutumia mbegu bora, utunzaji wa mashamba kwa usahihi, matumizi sahihi ya viuatilifu na kujifunza mbinu mpya za kilimo kupitia tafiti za kisayansi,” amesema Sharifa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi za TCB, asilimia 75 ya pamba inayozalishwa nchini huuzwa nje ya nchi ikiwa ghafi, hasa katika masoko ya Asia na Ulaya, hii inaifanya sekta ya pamba kuwa miongoni mwa bidhaa za kimkakati katika kukuza pato la taifa kupitia sekta ya kilimo.
Sharifa amesema pamba hulimwa zaidi katika mikoa 17 nchini, hasa Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Simiyu, Mwanza, Geita, Shinyanga na Tabora, Kanda ya Mashariki ni Morogoro, Tanga na Pwani, ambapo zaidi ya wakulima milioni Moja wanategemea zao hilo kama chanzo kikuu cha kipato.
Kwa mujibu wa ripoti ya maendeleo ya sekta ya pamba ya TCB, mikakati ya kukuza sekta ya ya pamba mbegu bora zisizo na nyuzi (kipara), zimeendelea kusambazwa kwa wakulima kwa lengo la kuongeza uzalishaji.
Pia, vituo vya kukusanya na kuchambua pamba (ginneries) vinaendelea kuboreshwa,mikakati ya kuongeza viwanda vya nguo na usindikaji wa pamba nchini inaendelea kuimarishwa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ambapo imenunua matrekta na ndege nyuki za kunyunyizia mashamba makubwa ya pamba .
“TCB inaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wakulima kupitia maofisa ugani ili kuhakikisha zao la pamba linazalishwa kwa tija na viwango vya kimataifa na kuweza kushindana katika soko,”amesema Sharifa.
Ofisa Kilimo huyo alitoa wito kwa wakulima wote wa pamba kuchangamkia fursa za mafunzo na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa maofisa wa TCB waliopo kwenye maonesho ya Nane Nane, ili kuongeza uelewa wao wa kilimo bora na kuongeza kipato kupitia uzalishaji wenye tija.
“Elimu tunayoitoa hapa ni bure, lakini thamani yake ni kubwa kwa mustakabali wa maisha ya mkulima na maendeleo ya taifa,” amesisitiza Sharifa.