Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa Richard Toyota akizungumzia kazi wanazozifanya katika maonesho ya Nanenane Jijini Mwanza.
Meneja wa Mamlaka ya Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Ziwa Richard Toyota akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Nanenane Jijini Mwanza
………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewaasa wananchi wanaojihusisha na shughuli za kilimo kukata bima ili kuweza kujilinda na majanga mbalimbali ikiwemo ukame.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TIRA Kanda ya Ziwa, Richard Toyota alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Wakulima Nane Nane ambapo kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanafanyika Nyamh’ongolo Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.
Alisema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa taasisi hiyo kutoa elimu ya bima kwa wananchi hususani wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali wadogo.
“Tunawahamasisha wananchi, taasisi na watoa huduma kusajiliwa na TIRA ili mifumo ya bima ifanye kazi kwa ufanisi.pia tupo hapa kusaidia wajasiriamali na wananchi wanaotaka kuwa mawakala au madalali wa bima kusajiliwa moja kwa moja,” Alisema Toyota.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imejiwekea lengo ifikapo mwaka 2030, asilimia 80 ya Watanzania wawe na uelewa wa bima na angalau asilimia 50 wawe wanatumia huduma hizo, ikiwa ni mkakati wa kulinda rasilimali na kukuza uchumi wa taifa”, Alisema Toyota
Aliongeza kuwa licha ya Watanzania wengi zaidi ya asilimia 70 kutegemea kilimo, mifugo, uvuvi na misitu, bado huduma za bima kwenye sekta hizi hazijapenya ipasavyo huku akiongeza kuwa kwa Kanda ya Ziwa pekee, takriban watu milioni 9.8 wanajihusisha na shughuli hizo, lakini idadi ya waliokata bima ni chini ya milioni 5.
Aidha, alieleza kuwa bima za kilimo na mifugo sasa zinaweza kutolewa kwa uhakika zaidi kutokana na uwepo wa skimu mbalimbali za serikali kama BBT na TWAISI, zinazosaidia kupunguza hatari zinazowakatisha tamaa wakulima na wafugaji.
Afisa Bima wa Reliance Insurance jijini Mwanza, Endrew Gabana, alisema bima ya kilimo imegawanyika katika makundi mawili bima ya mazao ya biashara na mazao ya chakula na inalenga kumlinda mkulima dhidi ya majanga ya ukame, magonjwa, wadudu na mvua nyingi.
“Bima hii humkinga mkulima tangu anapoanza shughuli za kilimo, ikitokea changamoto kabla ya mavuno, bado anapata fidia,” alisema Gabana.
Kwa upande wake, Alphonce Paul kutoka NIC Insurance ameeleza kuwa bima ya mifugo, hutoa kinga dhidi ya wizi, ajali na uchinjaji wa lazima wa mifugo kwa ushauri wa daktari,hasa pale panapokuwa na hatari ya kuenea kwa magonjwa.