Na John Bukuku – Nane Nane, Dodoma
Mamlaka ya Afya ya Mimea Tanzania (TPHPA) imezindua teknolojia mpya na ya kisasa ya kudhibiti visumbufu vya mazao, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wake katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 6, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema teknolojia hiyo inatumia mfumo wa uchunguzi wa vinasaba (DNA) ili kubaini kwa haraka aina ya wadudu na magonjwa yanayoshambulia mazao ambapo majibu hutolewa ndani ya dakika ishirini bila kuhitaji maabara
Profesa Ndunguru amesema kifaa hicho pia kina uwezo wa kutambua koo au jamii ya wadudu kwa usahihi ili kurahisisha uteuzi sahihi wa viuatilifu vinavyohitajika katika kudhibiti visumbufu hivyo
Aidha, kifaa hicho kina uwezo wa kubaini magugu vamizi pamoja na asili yake na tarehe yalipoanza kuonekana nchini sambamba na kupima ubora wa mbegu na kubaini magonjwa yanayoathiri mimea, mifugo, wanyamapori na hata binadamu
Kifaa hicho pia kinaweza kutumika kufanya uchunguzi wa vinasaba katika matukio ya ajali au uhalifu kutoa taarifa kuhusu ubora wa maji yanayotumiwa na binadamu na pia kusaidia kuzuia ujangili kwa kutambua wanyama waliopo kwenye hifadhi kwa kutumia DNA zao
Profesa Ndunguru amesema kuwa Tanzania ndiyo nchi ya kwanza duniani kuanzisha matumizi ya kifaa hicho katika sekta ya kilimo na kwamba TPHPA tayari imepokea vifaa 20 ambavyo vitasambazwa katika kanda zote za nchi ili kuanza kuwahudumia wakulima
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wakulima kwa kuwa itahakikisha usalama na ubora wa mazao ya biashara yanayosafirishwa nje ya nchi kwa kutambua asili ya bidhaa na kuzuia udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu
Wananchi waliotembelea banda la TPHPA katika maonesho ya Nane Nane wamepata fursa ya kuona kwa mara ya kwanza hatua za matumizi ya teknolojia hiyo ikiwemo uchukuaji wa sampuli kutoka kwenye mazao kama nyanya uchambuzi wa DNA na upatikanaji wa majibu ya visumbufu kwa muda mfupi
Teknolojia hiyo inatajwa kuwa chachu ya mageuzi ya sekta ya kilimo nchini kwa kuongeza tija kwa wakulima kupunguza hasara na kuimarisha nafasi ya bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa sambamba na kulinda rasilimali hai.