Na Seif Mangwangi, Kilimanjaro.
AWAMU ya kwanza ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Megawati 1.65 ambao pia unatarajiwa kutumika kufundishia wanafunzi wa chuo cha ufundi Arusha umefikia asilimia 75 na hivyo kuwa tayari kupokea wanafunzi wanaojifunza namna umeme wa maji unavyozalishwa.
Mradi huo unaojengwa katika eneo la Kikuletwa, Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa miradi mitatu inayofadhiliwa na benki ya dunia nchini kama vituo vya umahiri (Center of Excellency), ambapo pia miradi mingine inajengwa katika chuo cha ufundi DIT na chuo cha usafirishaji cha NIT huku miradi mingine ikitekelezwa katika nchi za Kenya na Ethiopia.
Kufuatia hatua hiyo, Disemba mwaka huu 2025, wanafunzi zaidi ya 600 wanatarajiwa kuanza masomo yao katika kampasi hiyo ya Kikuletwa ambapo mbali ya kujifunza umeme huo unaotengenezwa kwa njia ya maji, pia watajifunza umeme unaotokana na jotoardhi, umeme wa jua, na upepo.
Akizungumza jana katika kampasi ya Kikuletwa ambapo viongozi kutoka Baraza la Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki pamoja na Mkurugenzi wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi Dkt Frederick Salukele walitembelea eneo hilo la mradi, Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha, Profesa Mussa Chacha amesema miundo mbinu yote ya kupokea wanafunzi imekamilika ikiwemo mabweni ya kulala.
“ kila kitu kwaajili ya kupokea wanafunzi kipo tayari, tunatarajiwa kuanza na wanafunzi 600 ambao wanaenda kuanza masomo yao Disemba mwaka huu 2025, pia tumejenga jengo ambalo litapokea watu wazima wanaokuja kujifunza masuala ya umeme, “amesema.
Amesema chuo hicho pia kimeingia makubaliano na taasisi ya International Solar Alliance ambao wanatarajiwa kujenga kituo cha uzalishaji wa umeme wa solar katika kampasi hiyo ambapo wanafunzi pia watapata fursa ya kujifunza namna ya kuzalisha umeme wa njia ya solar pamoja na kutengeneza vifaa vya umeme wa solar.
“Taasisi hii ya kimataifa imekuwa ikihakikisha nishati jadidifu inasambaa kote duniani hivyo sisi kama ATC tumeingia nao makubaliano wanakuja kujenga kituo chao hapa lengo likiwa ni kufundisha wanafunzi namna ya kuzalisha umeme huo wa solar lakini pia watazalisha umeme ambao tutauuza TANESCO na umeme huu utakuwa mkubwa zaidi ya huu ambao tunaenda kuzalisha kwa njia ya maji,”amesema.
Mratibu wa Kanda wa mradi huo unaojulikana kwa jina la ESTRIP anayesimia miradi yote katika nchi za Kenya, Tanzania na Ethiopia ambae pia ni Mkurugenzi wa Baraza la vyo vikuu Afrika Mashariki Dkt Cosam Joseph amesema baada ya kukamilika kwa mradi huo wanategemea walimu na wanafunzi kutoka nchi mbalimbali Duniani kufika chuoni hapo kujifunza.
“Wanafunzi watakaotoka hapa watakuwa wameiva kiasi cha kuweza kwenda mahali popote duniani kusaidia miradi mingine ya uzalishaji wa umeme lakini pia kwa namna mradi huu unavyofanya vizuri tuna matumaini makubwa Benki ya Dunia itaendelea kufadhili miradi mingine katika sekta zingine ili kuleta tija kwa Taifa letu,”amesema Dkt Cosam Joseph.
Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ambaye pia ndio mratibu wa miradi hiyo ya ESTRIP Tanzania inayotekelezwa katika vyuo vya ufundi Arusha, NIT na DIT kutoka wizara ya Elimu na ufundi, Dkt Fredrick Salukele amesema kuanzia wiki ijayo Agosti 11 mitambo ya kuzalishia umeme itaanza kushushwa chini ya ardhi na hadi kufikia Aprili 2026 kazi ya kuzalisha umeme itaanza rasmi.
Amesema umeme utakaozalishwa katika kituo hicho utauzwa katika shirika la umeme la Taifa (TANESCO) na fedha zitakazopatikana zitatumika kuendeleza sekta hiyo chuoni hapo pamoja na kuanzisha ujenzi wa kituo kingine cha umeme katika eneo hilo hilo.
Dkt Salukele amesema mradi huo unaojengwa na kampuni ya kichina ya HNAC Technology Limited chini ya meneja msimamizi Yang Long pia inashirikiana na kampuni ya kitanzania ya White City Co. Limited ambayo inasimamisha na mhandisi Emmanuel Norbert ambaye pia alikuwa mwanafunzi katika chuo cha ufundi Arusha.
“Tunafurahi sana katika mradi huu wanaosimamia ni wafanyakazi ambao walishawahi kuwa wanafunzi katika chuo hiki hiki cha ufundi Arusha, pia msimamizi wa mradi huu kwa sasa mhandisi Robert Kabudi aliyekuwa akijenga bwawa la Mwalimu Nyerere, ni miongoni mwa wanafunzi waliosoma uhandishi chuoni hapa ATC na wasaidizi wake wote ni kutoka hapa hapa chuoni,”amesema.