Umoja na mshikamano imeelezwa kuwa ni silaha pekee ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ya kuimarisha mtangamano imara na wenye nguvu, utakaowezesha kufikia malengo yaliyowekwa na jumuiya hiyo.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kikao cha Maafisa Waandamizi wa SADC ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Balozi Albert Chimbindi alipokuwa anasoma hotuba ya ufunguzi ya kikao hicho jijini Antananarivo Agosti 06, 2025.
Katika kikao hicho ambacho ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban imeshuhudiwa Zimbabwe kupitia Balozi Chimbindi ikikabidhi uenyekiti wa kikao hicho kwa Madagascar ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Eric S. Ratsimbazafy alipokea na kuahidi kuendeleza yale yote mazuri yaliyoanzishwa na mtangulizi wake.
Balozi Chimbindi alisema katika kipindi cha uenyekiti wake, mtangamano wa SADC umeendelea kuimarika na mafanikio makubwa yamepatikana katika nyanja za ulinzi na usalama, utawala bora, maendeleo ya rasilimali watu, viwanda na huduma za jamii.
Alisema licha ya Kanda ya SADC kukumbwa na changamoto mbalimbali kama vile, ugonjwa wa UVIKO-19, ukame, maradhi, mabadiliko ya siasa za kimataifa na mabadiliko ya tabianchi, bado eneo hilo limeendelea kuwa imara kiuchumi.
Ametoa wito kwa nchi wanachama kuongeza jitihada za pamoja kujenga miundombinu ya barabara, reli, nishati na maji ili kuchochea shughuli za kiuchumi na biashara katika kanda.
“Kanda yetu imebarikiwa kuwa na vijana wengi pamoja na maliasili za kutosha, hivyo ni jukumu letu kuzitumia ipasavyo
kwa ajili ya kukuza uchumi na kuondoa tatizo la ajira kwa vijana”, Balozi Chimbindi alisema.
Kikao cha maafisa waandamizi ni moja ya vikao vya utangulizi kuelekea Kikao cha Baraza la Mawaziri Agosti 12 na baadaye Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliopangwa kufanyika Agosti,17, 2025.