Afisa kutoka Idara ya Uchambuzi wa Sera Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Fronto Furaha, akitoa elimu ya Sera za Fedha na Uchumi kwa wakazi wwa jiji la Dodoma, walipofika kutembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.
Afisa Habari Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Eva Valerian, akimweleza Mwananchi wa jiji la Dodoma, Bw. Carlos David, kuhusu Majukumu yanayotekelezwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, alipofika kutembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.
Mchumi Mwandamizi kutoka Idara ya Bajeti ya Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Eliud Mkiramweni, akimweleza mkazi wa jiji la Dodoma, Bw. Justus Marco, kuhusu namna maandalizi ya Bajeti ya Serikali yanavyotekelezwa, wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.
Mchumi Mwandamizi, Wizara ya Fedha, Bw. Erick Mang’era, akitoa elimu jinsi ya kukuza na kuendeleza biashara pamoja na usimamizi binafsi wa fedha, kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Makole, walipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.
Afisa Hesabu kutoka Kitengo cha Huduma za Mfuko Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Mercelina Haule, akitoa ufafanuzi kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko Mkuu, kwa mkazi wa jiji la Dodoma, Bi. Dorothea Bugenyi, wakati alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
……..
Josephine Majura na Joseph Mahumi WF, Dodoma
Wananchi wametakiwa kujenga utamaduni wa kufuatilia kwa karibu mchakato wa maandalizi ya bajeti ya Serikali ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Mchumi Mwandamizi wa Idara ya Bajeti ya Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Eliud Mkiramweni, alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.
Akizungumza katika Banda la Wizara ya Fedha, Bw. Mkiramweni alieleza kuwa bajeti ya Serikali haipaswi kuangaliwa tu kama chombo cha kugharamia shughuli za kiserikali, bali ni dira inayoonesha vipaumbele vya Taifa ambavyo vinaweza kuwanufaisha wananchi kiuchumi.
“Kila mwaka Serikali huandaa bajeti ambayo huainisha maeneo ya kipaumbele kama vile miundombinu, kilimo, afya, elimu, maji, nishati, biashara ndogo na za kati pamoja na mazingira, wananchi wakijua haya mapema, wanaweza kutumia fursa zilizopo kuboresha maisha yao,” alisema Bw. Mkiramweni.
Alisisitiza kuwa mchakato wa bajeti ni wazi kwa umma na huanzia ngazi ya kijiji hadi kufikia Bunge, hivyo ni muhimu wananchi wakashiriki katika hatua zote kwa kupendekeza miradi, kufuatilia kiasi cha fedha kinachotengwa, na kuangalia utekelezaji wake.
“Mwananchi akihusika tangu mwanzo anakuwa na uwezo wa kudai uwajibikaji, kuelewa anachostahili, na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii yake,” alisema Bw. Mkiramweni.
Aliongeza kuwa ushiriki wa wananchi huongeza uwazi, uwajibikaji na kuibua fursa mpya za kiuchumi hasa kwa vijana, wanawake na wakulima wadogo.
Bw. Mkiramweni alisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kujihusisha si tu kwenye mikutano ya kupanga miradi, bali pia kwenye vikao vya halmashauri vinavyohusisha majadiliano ya bajeti, ambapo taarifa muhimu juu ya rasilimali na vipaumbele hutolewa.
Aidha, Bw. Mkiramweni aliwahimiza viongozi wa vijiji na mitaa kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa mchakato wa bajeti na kuwashirikisha ipasavyo wananchi wao katika kupanga vipaumbele vya maendeleo.
Aliongeza kuwa uelewa wa bajeti haupaswi kuwa kwa wasomi pekee au maafisa wa Serikali, bali kila Mtanzania mwenye dhamira ya kuona maendeleo katika jamii yake anapaswa kushiriki kikamilifu.
“Mchakato huu ni wetu sote, Bajeti ya Serikali ina matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi. Tukiwa na sauti kwenye upangaji wake, basi tutaona miradi yenye tija inayotekelezwa kwa ufanisi,” alifafanua Bw. Mkiramweni
Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi zilizo chini yake inashiriki katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025’’.