

Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha ACT-Wazalendo umeidhinisha kwa kishindo majina ya Luhaga Mpina na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, kuwa wagombea rasmi wa chama hicho kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katika kura za maoni zilizofanyika leo, Luhaga Mpina aliibuka mshindi kwa kupata kura 559 kati ya kura 605 halali zilizopigwa, sawa na asilimia 92.3. Mpinzani wake wa karibu, Aaron Kalikawe, alipata kura 46 tu, ambazo ni sawa na asilimia 7.7.

Kwa upande wa Zanzibar, Othman Masoud, ambaye alikuwa mgombea pekee, alipata kura za ndiyo 606 kati ya 610 zilizopigwa, sawa na asilimia 99.5. Kura tatu zilikuwa za hapana huku kura moja ikiharibika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya ACT-Wazalendo, Mbarala Maharagande, alisema idadi ya wajumbe waliopiga kura kwa upande wa urais wa Muungano ilikuwa 610, ambapo kura halali zilikuwa 605 na zilizoharibika tano.
Akifungua mkutano huo, Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, alisisitiza dhamira ya ACT-Wazalendo kuleta mabadiliko makubwa nchini kwa kuweka mbele ajenda ya uwajibikaji, haki, na maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote.
Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa ni kuwateua wagombea wa urais, lakini pia ulijadili masuala mbalimbali ya ndani ya chama ikiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.