Morogoro, 06 Agosti 2025;
Elimu ya huduma mahususi za hali ya hewa inayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuwavutia wadau wengi waliotembelea katika banda la TMA kupitia maonesho ya NaneNane 2025 yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya NaneNane, Morogoro.
“ Sikuwahi kufikiria kama TMA inauwezo wa kuniandalia utabiri katika maeneo ya shamba langu, kwa kweli imenivutia sana” Alizungumza hayo mmoja wa wadau waliotembelea banda la TMA kupitia maonesho ya NaneNane, Morogoro Ndg. Seif Sempanga, Mkulima mwenye Ekari zaidi ya 300, Kilindi Tanga.
Aidha, kupitia ujio wa wanafunzi kutoka shule mbalimbali mkoani Morogoro, wameshukuru
kupata elimu ya mchakato mzima wa uandaaji utabiri wa hali ya hewa, namna taarifa za hali ya hewa zinavyosaidia huduma za usafirishaji ikiwemo usafiri wa anga na maji pamoja na sekta ya utalii.
“Namshukuru Mungu nimekuja kutembelea banda la TMA, nimejifunza mengi ambayo mengine sikuwahi kufikiria kuwa TMA wanafanya kazi kubwa namna hii, kumbe uwepo wa mvua inasaidia sekta ya utalii kuneemeka katika upatikanaji wa wanyama wengi kutokana na uwepo wa malisho na maji ya kutosha” alisema hayo mwanafunzi Nusiata Alexanda, kidato cha tatu kutoka shule ya sekondari ya sharte, Morogoro.