Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene, pamoja na mpiga picha wa zamani wa Rais, Ikulu, Fredrick Maro, wamekabidhiwa rasmi Vitambulisho vyao vya Uandishi wa Habari (Presscard) leo tarehe 07 Agosti 2025, baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa Sheria.
Zoezi hilo limefanyika katika Ofisi za Bodi zilizopo Mtaa wa Jamhuri, jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula.
Akizungumza mara baada ya kuwakabidhi vitambulisho hivyo, Wakili Kipangula alibainisha kuwa Mwambene na Maro wamefuata utaratibu wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kujisajili, kuthibitisha taaluma zao na kuwasilisha nyaraka zilizotakiwa.
“Hili ni zoezi endelevu. Waandishi wote wa habari nchini wanatakiwa kuwa na Presscard inayotolewa na Bodi ya Ithibati ili kuendesha shughuli zao za kihabari kihalali na kuzingatia maadili ya taaluma na Sheria,” alisema Kipangula.
Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, kifungu cha 19 (1), mtu yeyote anayetaka kufanya kazi za kihabari ni lazima awe amesajiliwa rasmi na Bodi, kuthibitishwa na kupewa kitambulisho kinachotambulika na Serikali. Vinginevyo, mtu anayejihusisha na shughuli za kihabari bila kuthibitishwa kisheria anakuwa anatenda kosa.
Assah Mwambene, ambaye pia amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Habari katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa, ni mmoja wa Waandishi wa habari wenye uzoefu mpana katika sekta ya mawasiliano na diplomasia ya umma. Fredrick Maro pia ni mpiga picha maarufu aliyekuwa karibu na taasisi ya Urais kwa miaka kadhaa, na mchango wake umetambuliwa mara nyingi katika vyombo vya habari na kumbukumbu za taifa.
Wakati huo huo, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imeendelea na kampeni ya kuwasisitiza waandishi wote wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali kuhakikisha wanajisajili, kuthibitishwa, na kufanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma yao.
“Tunapenda kuona taaluma ya habari ikiheshimika, na hilo linaanza na kila mwandishi kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Sheria. Hii inalinda hadhi ya taaluma na maslahi mapana ya taifa,” aliongeza Wakili Kipangula.
Mpaka sasa ya waandishi wa habari 3,240 wameshajisajili, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kutokana na mabadiliko yanayoendelea ndani ya vyombo vya habari na utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa Ithibati.