Na Mwandishi wetu, Kiteto
MBUNGE aliyemaliza muda wake wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, Wakili msomi, Edward Ole Lekaita Kisau ameongoza kura za maoni ya CCM kwenye nafasi ya ubunge kwa kupata kura nyingi 12,532 kuliko mgombea yeyote nchini.
Wakili msomi Ole Lekaita ameweka historia kwa mwaka 2025 ya kuwa mgombea ubunge nchini wa CCM kupata kura nyingi kuliko mwingine.
Katibu wa CCM wilaya ya Kiteto, Denis Mwita akisoma matokeo ya kura za maoni kwenye kata zote 23 za eneo hilo, amesema Ole Lekaita amepata kura 12,532.
Mwita amesema nafasi ya pili imeshikwa na mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia wilaya ya Kiteto Sisca Seuta ambaye amepata kura 1,919.
Amesema nafasi ya tatu imeshikwa na mgombea Boniface Hindi ambaye amepata kura 1,294.
Amemtaja aliyeshika nafasi ya nne ni mgombea Alais Nangoro ambaye amepata kura 753.
Mkazi wa kata ya Sunya Kulwa Mkamba amempongeza Ole Lekaita kwa ushindi huo mkubwa ambao umekuwa historia Kiteto kwa mgombea huyo kupata kura nyingi.
Mkamba amesema wakili msomi Ole Lekaita amewashinda hata mawaziri, manaibu mawaziri, kwa kura nyingi kwani hakuna mgombea ubunge aliyepata kura hizo katika jimbo lake.
“Isaya 60 maandiko yanasema inuka uangaze kwa kuwa nuru yako imeng’aa na utukufu wa Mungu umekuzunguka, kwenye uchaguzi huu vijana wa CCM Kiteto tutashinda kitaifa kura za Rais Samia Suluhu Hassan, Ole Lekaita na madiwani,” amesema Mkamba.