
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) Bw. Erasto Mulokozi akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika leo Agosti 7, 2025 jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kosuri akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deogratius Balile akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika leo Agosti 7, 2025 jijini Dar es Salaam.



Wahariri na waandishi wa habari wakiwa katika kikao kazi na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) Bw. Erasto Mulokozi.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umetangaza ongezeko la kiwango cha uagizaji wa mafuta nchini kupitia Mfumo wa Uagizaji kwa Pamoja (Bulk Procurement System – BPS), ambapo kufikia mwaka 2024 kiwango hicho kimefikia tani 6,365,986 kutoka wastani wa tani 5,805,193 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 9.6.
Akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika leo Agosti 7, 2025 jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Mulokozi, amesema kuwa hadi kufikia Desemba 2025, inatarajiwa kuwa kiasi cha tani 7,090,165 kitakuwa kimeagizwa, ongezeko la asilimia 11.4 ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Bw. Mulokozi ameeleza kuwa maboresho yaliyofanyika yameongeza ufanisi wa mfumo huo, na hivyo kuimarisha imani ya mataifa jirani katika kutumia mfumo huo kwa ajili ya uagizaji wa mafuta ghafi.
Takwimu zinaonesha mwaka (2021–2025): 2021: Tani milioni 5 ziliagizwa, ambapo tani milioni 2 zilipelekwa mataifa jirani na milioni 3 kwa matumizi ya ndani, 2022: zaidi ya tani milioni 6 ziliagizwa; tani milioni 3 kwa mataifa jirani, zaidi ya milioni 2 kwa matumizi ya ndani, 2024: tani zaidi ya milioni 6 ziliagizwa; tani milioni 3 kwa matumizi ya ndani na zaidi ya milioni 3 kwa mataifa jirani. Januari–Septemba 2025: tani zaidi ya milioni 5 ziliagizwa; milioni 3 kwa mataifa jirani na zaidi ya milioni 2 kwa matumizi ya ndani.
Aidha, amesema kuwa idadi ya kampuni za mafuta imeongezeka kutoka 33 mwaka 2021 hadi 73 mwaka 2025, na ongezeko hilo linatoa fursa zaidi za ajira kwa Watanzania katika sekta mbalimbali zinazohusiana na nishati.
Vilevile, nchi mbalimbali zikiwemo Zambia, Burundi, Rwanda, Malawi, na hata Kenya zimekuwa zikija kujifunza kuhusu Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja wa Tanzania kutokana na mafanikio na ufanisi wake.
“Mfumo huu unaendelea kuaminika na kuimarika. Ni mafanikio makubwa kwa nchi yetu kuona kuwa hata mataifa jirani yanakuja kujifunza kutoka kwetu,” amesema Bw. Mulokozi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri, ameeleza kuwa Msajili wa Hazina anathamini juhudi za wanahabari nchini na ataendelea kushirikiana nao kwa karibu katika kuhabarisha umma na kudumisha uzalendo.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deogratius Balile, amepongeza mfumo wa BPS kwa kuboresha upatikanaji wa mafuta ghafi nchini na kusisitiza umuhimu wa kudhibiti ubora wa mafuta yanayoagizwa kupitia mfumo huo.